Tuesday, 1 May 2018

SIMAMA KATIKA NAFASI YAKO KUMTUMIKIA MUNGU.

BWANA YESU ASIFIWE

Kwaajili ya sifa na utukufu wa Mungu Baba kwa jina la Yesu Kristo nakuletea somo lenye kichwa kinachosema,

SIMAMA KATIKA NAFASI YAKO KUMTUMIKIA MUNGU.

Dunia imesimama katika nafasi yake huku yule mwovu naye akisimama imara kuhakikisha kwamba anawapata walio wake.
Lakini inatubidi na sisi tuliofanyika kuwa wana wa Mungu tusimame imara kuhakikisha kwamba tunamshinda kwa kuwafungulia dhambi wale waliofungwa.
Ni wazi kwamba unaposimama katikati ya mataifa na kuongea kweli kuhusu huyu Yesu utapingwa na kudhihakiwa na wengi lakini tusife moyo wana wa Mungu.

TWENDE KWENYE NENO LA MSINGI WA MAFUNDISHO YETU.

MATHAYO 5:11-12
Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu.

Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.

****************

Wakati unapomtamka Mungu huwa shetani haimpi shida yoyote na hata watu watakusikiliza kwa makini sana kana kwamba wanataka kujifunza.
Hata shetani anajijuwa kabisa hawezi kupambana na Mungu, anajijuwa pia hana uwezo wa kupambana na Yesu.
Anachojitahidi yeye ni kuhakikisha anaweka uvuli kwa hao unaowahubiria ili tu wasije wakaikubali hiyo damu ya Yesu ambayo iko katika wokovu.
Hataki kwenda jehanamu peke yake.

Utasemwa vibaya kwaajili ya jina la Yesu na hata tunaona namna ambavyo hata baadhi ya huduma zetu zinavyopigwa vita na anadhiriki kutengeneza hata manabii wake wa uongo na wanapofanya jambo lililo kinyume analifanya lijulikane na kila mtu ili hilo jambo liwe sababu ya watu kutokuziamini huduma nyingine za Yesu Kristo.
Jiulize ni kwanini mtumishi wa kweli anapofanya jambo jema asiongelewe na kujulikana na kila mtu?

Lakini hata kama ukisemwa vibaya na watu kuanza kukufikiria kwa namna yao wewe endelea kuhubiri tena kwa bidii zaidi maana ndicho kilichomfanya Mungu akuite kwa jina lake.

1WAKORINTHO 15:58
Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana.

***************

Tuendelee kuchapa injili ya Yesu na kumfikishia habari kila mmoja ili baadae asije akajitetea kwamba hakusikia.
Utachekwa mara nyingi sana kuonekana masikini uliyekosa Kazi lakini nakuambia hutachekwa bure.
Yani wanadamu wamekuwa wa ajabu sana.

Unaweza ukawa umesimama mahali unahubiri halafu pembeni yako akawa amesimama kahaba aliyevaa nguo za aibu yuko uchi mwili mzima lakini utashangaa kati yenu wawili watu wanakuona wewe ndiye kituko.
Mungu atusaidie sana tuendelee maana hii kazi siyo bure.
Ipo siku ile moja tu ya kupepeta makapi na ngano na hapo wako watakaolaani hata matumbo ya mama zao na wote watatamani kama wangehubiri.
Sisi tunaoijuwa kweli hatutaki mtu ajute siku hiyo na ndiyo maana huwa tunahangaika kuhakikisha watu wanampokea Yesu na kuachana na dhambi.

2WAKORINTHO 4:3-4
Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea;

Ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.

********************

Huyu shetani anaakili nyingi sana mpaka Mungu anamtunuku jina
 (mungu wa dunia hii)
Fikra za watu zimepofushwa hawataki kabisa kuipokea injili ya kweli.
Mtu akilazimika saana basi atamkiri Yesu lakini atakuambia lakini mimi siiachi dini yangu.
Shetani ni mbaya mno.
Anakuambia tu Mungu haangalii dini au unakoabudu bali anaangalia moyo.
Analiongea andiko kuubwa kwa namna ya kawaida kabisa na anajiona yuko sahihi.
Mpendwa usije ukafikiri kuna mtu aliyeokoka na bado yuko kwenye dini na wala usidhani hizi dini zilizopo unazodhani zinamwabudu Mungu kwamba ipo hata moja Mungu anayopendezwa nayo.
Ni mungu wa dunia hii anapofusha fikra zako.
Angalia hata hilo jina mungu limeandikwa kwa kuanza na herufi ndogo likimaanisha kwamba anayetajwa hapo ni shetani ibilisi.

Unavyokataa injili ya Yesu usidhani hata kama angekuja nabii wa zamani ungemwelewa.
Tatizo lililopo kwako siyo Yule anaekuhubiria bali ni huyo anayekuzuia wewe kuelewa ili usije ukoelewa ukaokoka akakukosa.

YEREMIA 1:5-10
 Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.

Ndipo niliposema, Aa, Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto.

Lakini BWANA akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru.

Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema BWANA.

Ndipo BWANA akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; BWANA akaniambia, Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako;

Angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung?oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.

******************
Huyu nabii Yeremia alipata wakati mgumu sana katika kipindi chake.
Lakini ukisoma maandiko ukimfuatilia jinsi Mungu alivyomwahidi huthanii kama ndiye huyo anaepitia changamoto kubwa namna hii.
Nikimsoma huwa napata nguvu ya kumhubiria mtu yeyote.
Mungu alimthibitishia kabisa mwamba ametia maneno yake kinywani mwa Yeremia.
(yaani akiongea ni Mungu kaongea)
BWANA YESU ASIFIWE SANA.

YEREMIA 20:7-9
Ee BWANA, umenihadaa, nami nimehadaika; wewe una nguvu kuliko mimi, ukashinda; nimekuwa kitu cha kuchekesha, mchana kutwa; kila mtu hunidhihaki.

Maana kila ninenapo napiga kelele, nalia, Dhuluma na uharibifu! Kwa kuwa neno la BWANA limefanywa shutumu kwangu, na dhihaka, mchana kutwa.

Nami nikisema, Sitamtaja, wala sitasema tena kwa jina lake; basi, ndipo moyoni mwangu kumekuwamo kama moto uwakao, uliofungwa ndani ya mifupa yangu, nami nimechoka kwa kustahimili, wala siwezi kujizuia.

*****************
Cha kushangaza kila Yeremia alipopewa unabii kwaajili ya taifa la Israeli watu walimdhihaki na kumwona kituko.
Mpaka Yeremia anadhiriki kumwambia Mungu kwamba amemhadaa.
Lakini siyo kweli kwamba Mungu alimhadaa.
Watu wanamshutumu wanamwona si kitu mbele yao.
Alitamani sana aache kuongelea habari za Mungu kabisa lakini haikuwa rahisi.

Watu wanafikiri labda sisi tunatumia muda wetu mwingi kuwahubiria ili tupate kitu kutoka kwao.
Hayo ni mawazo kamili ya shetani.
Wewe unaehubiriwa siku ukiijua kweli halafu ukamhubiria mtu akakataa utatamani hata umpige lakini sisi huwa tunampiga na upanga ambao ni neno la Mungu.
Vita vyetu si ju ya damu na nyama bali ni katika falme na mamlaka.
Utatamani kumpiga maana anavyoikataa kweli uliyofundishwa na Yesu unamwona kama mfu lakini yeye anakuona wewe ndiye kichaa.

Yeremia anasema sitamtaja tena Mungu maana natukanwa na kufanyiwa kila aina ya dhihaka.
Lakini anaposema hatamtaja ndivyo anavyozidi kuumia zaidi anapoona watu wanapotea huku yeye akiijuwa njia.
Ndugu zangu sisi tunaoijuwa kweli tunapokueleza ukapuuza huwa tunaugua haswa.
Tuoneeni huruma muokoke mtatuuwa.

Huwa kweli tunahisi kama moto unawaka ndani yetu.

WAEBRANIA 12:29
Maana Mungu wetu ni moto ulao.

***************

Lile neno la kweli linapokaa ndani yetu halafu tukaamua kunyamaza kwaajili ya kejeli na matusi yenu huwa linatulazimu kutoka kivyovyote maana Mungu huwa haliweki ndani yetu ili likae bila kuponya watu.

Mimi sitaacha kufundisha injili ya kweli hata iweje na wala siwezi kunyamaza.
Nitasimama katika nafasi yangu na panapohitajika neema ya Yesu basi itashuka.

Usiache kabisa kuifanya Kazi ya Mungu kwaajili ya wanadamu.
Mungu anapokutuma kwenda kuifanya huwa anajuwa kila kitu mwisho wake kabla hata wewe hujaujua mwanzo.
BWANA YESU ASIFIWE SANA.

EZEKIELI 2:5-6
Nao, kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia, (maana ndio nyumba ya kuasi hao), hata hivyo watajua ya kuwa nabii amekuwako miongoni mwao.

Na wewe, mwanadamu, usiwaogope hao, wala usiyaogope maneno yao, ijapokuwa miiba na michongoma i pamoja nawe, nawe unakaa katikati ya nge; usiyaogope maneno yao, wala usifadhaike kwa sababu ya nyuso zao, wajapokuwa ni nyumba yenye kuasi.

*****************
Mungu anawajuwa kabisa.
Wako watakaoielewa hiyo injili lakini wanaamua kuwa na mioyo migumu kwa makusudi kwakuwa wana mambo yao na wanadhani hawawezi kuyaacha na hayachangamani na wokovu.

Mungu anajuwa kabisa huko alikokutuma na kwa watu walioasi na anakuambia kuwa usifadhaike kwaajili ya hayo utakayotendewa ikiwa wamekukataa wewe kung'uta mavumbi ya miguu yako uyaacha pale.
Daima endelea kusimama katika nafasi yako sawasawa hata katika marafiki zako na ndugu na jamaa asije akawepo hata mmoja akaja kukulaumu kwamba hukumwambia.

EZEKIELI 33:7-9
Basi wewe, mwanadamu, nimekuweka kuwa mlinzi kwa nyumba ya Israeli; basi ulisikie neno hili kinywani mwangu, ukawape maonyo yangu.

Nimwambiapo mtu mbaya, Ewe mtu mbaya, hakika utakufa, nawe husemi neno la kumwonya mtu huyo, aiache njia yake, mtu mbaya huyo atakufa katika uovu wake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako.

Walakini ukimwonya mtu mbaya kwa sababu ya njia yake, kusudi aiache; wala yeye asiiache; atakufa huyo katika uovu wake, lakini wewe umejiokoa roho yako.

****************

Mpendwa kama neno la Mungu likijaa ndani yako sawasawa hutapata nafasi ya kulala bali utakuwa unalia kila wakati kwa wale wanaolikataa.
Lutu aliwaambia wakwe zake twendeni tuondoke maana huu mji utaangamizwa, lakini alikuwa kama kichekesho kwao wakadharau na baadae waliangamia katika ule moto.
Vivyo hivyo Nuhu alipokuwa akijenga safina alionekana kichekesho lakini baadae walewale waliokuwa wakimcheka waliangamia.

Usipowaambia watu ukweli kuhusu Yesu ujue utahukumiwa wewe.
Bali ukiwaambia wakikataa watajihukumu wenyewe.

NEHEMIA 5:19
Unikumbukie, Ee Mungu wangu, kwa mema, yote niliyowafanyia watu hawa.

******************

Wala usijali utakapowaambia wakakataa, wewe waambie huku ukiendelea kumwomba Mungu atakukumbuka kwa wakati wake.
Mwisho wa ubaya ni aibu pia karama ya dhambi ni mauti lakini pia wema hauozi wewe dimana katika nafasi yako.

UFUNUO 22:11-12
Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa.

Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.

*****************

Zidi kuitenda haki ya Mungu na mwenye kuacha matendo mabaya na ayaache na anayechagua matendo mabaya na aendelee lakini muda wa kujuta upo kabisa.
Ujira wako upo endelea kumwamini Mungu naye atakulipa kama Kazi yako ilivyo.
Chapa injili tena ikiwezekana pita nyumba hadi nyumba na ukifukuzwa ndipo unazidi kuinuliwa.
Cha msingi tu wewe unapoenda kwa mtu omba kibali kwa Mungu ili akupe msaidizi usiende peke yako.
Kazi yako wewe ni kuhubiri injili ya kweli lakini kuokoa muachie Yesu.

YOHANA 14:16-18
Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele;

Ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.

Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu.

**************
Unapoenda kuhubiri ukiwa na huyo Roho ambaye ni msaidizi atalithibitisha neno mioyoni mwao na wakiamua kuokoka wataokoka lakini wakiamua kugeuza mioyo yao kuwa migumu basi mshukuru Mungu na uwe unawaombea.
Usipofanya hivyo utajikuta hata wokovu ulionao unakosa nguvu hata baadae kuanguka kabisa.

YOHANA 15:1-5
Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima.

Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa.

Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia.

Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu.

Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.

***************

Yesu anajifananisha na mti wa mzabibu halafu baba yake ni mkulima.
Unapokuwa umeokoka unakuwa ni tawi katika ule mti wa mzabibu.
Na ni kweli kwamba mkulima yeyote anapotaka mti uzae vizuri huwa anatoa yale matawi dhaifu ili yasiyanyime yale matawi imara nafasi ya kuzaa vyema.
Ukikaa ndani ye Yesu sawasawa naye atakaa ndani yako na atakupa Roho msaidizi na ukimhubiria mtu ni lazima ataokoka.
Anaweza asiokoke siku hiyo lakini Yesu ambae ni neno likikaa ndani yako litakuelekeza kumwombea na ipo siku lile neno ulilomwambia litakuja kuhuishwa na Roho mtakatifu ndani yake na ataokoka.
BWANA YESU ASIFIWE SANA.

Huwezi ukasema umeokoka huku unamficha huyo Yesu wako wala humshuhudii kwa watu.
Kama huna jitihada za kuwafanya wengine waokoke ujue wokovu wako uko mashakani na wewe utakatwa maana ni tawi lisilozaa.
Yesu hajakuokoa tu bali amekuokoa ili akutumie katika ufalme wake.

Watu ambao shetani anawatumia wanafanya Kazi kwa bidii usiku hawalali na hawapati chochote sasa inashangaza sana wewe unaetumika na Mungu tena umeokolewa unasemaje umeokoka halafu upoupo tu?
Hakuna wokovu wa namna hiyo inabidi ubadilike na ujitathimini na wokovu wako uko wapi.

ASANTE SANA MUNGU BABA WA BWANA WETU YESU KRISTO NA ROHO WAKO MTAKATIFU ULIYE MFANYA KUWA MSAIDIZI NDANI YANGU KATIKA SOMO HILI.
NAOMBA PIA HILI SOMO LIKAHUISHWE KATIKA MIOYO YA WATU WAKO KWA JINA LA YESU KRISTO.
Ameeeen

#Powered_By_Holly_Spirit

2 comments:

  1. Mungu akubariki mtumishi wa Mungu binafsi nimebarikiwa saaana

    ReplyDelete
  2. Thank You and that i have a tremendous present: How Much Should House Renovations Cost old house renovation

    ReplyDelete