Saturday, 19 February 2022

UFAHAMU MBAYA KUHUSU NENO LA MUNGU NDIYO MAUTI YENYEWE!

 UFAHAMU MBAYA KUHUSU NENO LA MUNGU NDIYO MAUTI YENYEWE!


Nisikilize wewe mwamini! 


Hatua ya kuanza kumwazia Mungu mabaya ni chanzo cha mauti yako! 


Unapomfikiria Mungu kuwa anaweza kuwa chanzo cha mambo mabaya hapo unajitengenezea kichaka cha adui/Shetani kujificha na kukutandika sawasawa! 


1 YOHANA 1:5

Na hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba Mungu ni nuru, wala giza lo lote hamna ndani yake.


Kitu pekee kilicho kwa Mungu ni nuru tu, wala hashirikiani na giza, adui anapokuona unaanza kufikiri kuwa Mungu analeta mabaya kwako basi ujue anapata nafasi ya kukutandika ili umchukie Mungu


Ni kawaida sana kumsikia mlokole akisema eti Mungu amempitisha katika mambo mabaya ili ampe mema!!! 


Mungu hana tabia ya kumtesa mtu ili ampe mema


Wewe kama kuna mabaya unapitia basi uwe na uhakika umeyatengeneza mwenyewe


Usianze kusimulia mahadithi yako kisha ukayaita ushuhuda wa namna ambavyo Mungu alikua anakuandaa ili akupe hicho ulichokipata! 


Yesu anasema ikiwa nyinyi mlio waovu mnaweza kuwapa watoto wenu vipawa vyema, si zaidi sana kwa Baba yenu aliye mbinguni? 


Kama wewe huwezi kumtesa mtoto wako ndipo umpe yaliyo mema ni kwanini ufikiri kwamba Mungu anaweza kuwafanyia watoto wake hivyo? 


Au unajiona wewe ni mwema sana kuliko Mungu? 


Acha kiburi uwe na nidhamu unapomwongelea Mungu


Usiokote okote maneno na kuyaunganisha unganisha kisha ukaanza kuwafundisha watu kuhusu tabia ya Mungu


Mashida shida yako uliyopitia kwaajili ya uchaguzi na maamuzi yako mabovu hayajawahi kuwa injili yenye kuokoa hata siku moja


Kinachofanya watu waokoke ni injili maana ndiyo yenye uweza wa Mungu uletao wokovu


Wala habari mbaya zilizokupata wewe hazikuwahi kuweza kuokoa na kumfanya mtu aokoke utakapomsimulia


Injili ni habari njema, ni kuhusu ufufuo wa Yesu Kristo tu na roho wa Mungu kukaa ndani ya anayeamini huo ufufuo! 


Inatosha tu kusema hivyo, acha kutishia watu kwa hadithi za kutisha


Habari za Mungu hazitishi watu bali zinaleta amani kwa kila asikiaye


Ukiona unahubiri halafu watu wanaona wokovu ni mgumu basi ujirekebishe maana hiyo siyo injili! 


Inatosha kusema hivyo! 


Kristo anafunuliwa! 


Kristo anatukuzwa!

No comments:

Post a Comment