Saturday 28 April 2018

BWANA NI NGOME SIKU YA TAABU

BWANA YESU ASIFIWE

Kwa kusudi na uwezo wa Roho Mtakatifu leo nakuletea somo lenye kichwa kinachosema, 

BWANA NI NGOME SIKU YA TAABU

Hakika Mungu wetu ni mwaminifu na hatamwacha mtu wake aangamie. 

MSINGI WA MAFUNDISHO YETU

NAHUMU 1:7
BWANA ni mwema, ni ngome siku ya taabu; naye huwajua hao wamkimbiliao.

***************

Mungu anaposema kwamba yeye ni ngome siku ya taabu ni kwamba hakuna jambo linaloweza kukutokea hata kama linatisha kiasi gani halafu Mungu asiwepo kukutetea. 

Mungu anajiita yeye ni ngome akimaanisha ni ulinzi mkubwa sana kwako na anakujuwa wewe umkimbiliae siku zote. 
Ikiwa yeye ni mwema basi anakuwazia mema kila wakati hivyo huna haja ya kuogopa maana pale tunakoishia ndiko yeye anakoanzia. 

Yapo mambo magumu sana na ya taabu yanayoweza kukutokea na ukashindwa kujuwa cha kufanya lakini pale tunaposema hapa basi huwa Mungu anaanzia hapo, haleluya. 

DANIELI 3:4-6
Ndipo mpiga mbiu akapiga kelele akisema, Enyi watu wa kabila zote, na taifa, na lugha, mmeamriwa hivi,

wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, lazima kuanguka na kuiabudu sanamu ya dhahabu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha.

Na kila mtu asiyeanguka na kuabudu atatupwa saa iyo hiyo katika tanuru ya moto uwakao.

****************

Siri ya Mungu kukuonekania siku ya taabu yako ni pale utakapokuwa umemwamini na kumkimbilia yeye. 

Mfalme Nebukadreza alitoa amri ya watu wote kuiabudu sanamu lakini Shedraka na Meshaki na Abednego waliokuwa maliwali huko wilaya ya Babeli walikataa wakamkimbilia Mungu ili awe ngome kwao kwa ile taabu iliyokuwa mbele yao. 
Walikiuka amri ya mfalme na kuamua kumkimbilia Mungu mpaka hatua ya mwisho. 
Halikuwa jambo rahisi sana kama ambavyo watu wanaweza kulichukulia. 

DANIELI 3:14-18
Nebukadreza akajibu, akawaambia, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, je! Ni kwa makusudi  hammtumikii mungu wangu wala kuisujudia sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha?

Basi sasa, kama mkiwa tayari wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, kuanguka na kuisujudia sanamu niliyoisimamisha, ni vema; bali msipoisujudia, mtatupwa saa iyo hiyo katika tanuru iwakayo moto; naye ni nani Mungu yule atakayewaokoa ninyi na mikono yangu?

Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza, hamna haja kukujibu katika neno hili.

Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme.

Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.

***********

Mfalme Nebukadreza alitoa tena kauli ya mwisho baada ya kusikia kuwa wamepuuza ile amri. 
Lakini Meshaki na wenzake walimjibu mfalme kwa ujasiri kwamba hatutakubali kuitumikia hiyo miungu yako. 
Na hata kama Mungu wetu hatatutetea hatutakubali kuitumikia hiyo miungu yako. 
Hiyo ndiyo maana ya kumkimbilia Mungu na kumwamini, haleluya. 

Mfalme alikasirika sana kwa majibu yao na akaamuru watupwe kwenye tanuru la moto. 

Kumbuka bado Waliendelea kumwamini Mungu na wakaamini kwamba Mungu wao hashindwi na chochote na waliendelea kumuomba juu ya adhabu iliyokuwa mbele yao. 

DANIELI 3:24-26
Ndipo Nebukadreza akastaajabu, akainuka kwa haraka; akanena, akawaambia mawaziri wake, Je! Hatukutupa watu watatu, hali wamefungwa, katikati ya moto? Wakajibu, wakamwambia mfalme, Kweli, Ee mfalme.

Akajibu, akasema, Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu.

Kisha Nebukadreza akaukaribia mdomo wa ile tanuru iliyokuwa inawaka moto. Akanena, akasema, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye juu, tokeni, mje huku. Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakatoka katika ule moto.

***************

Hapa ndiko shetani huwa anapowatingisha watu wa Mungu imani yao. 
Fikiri ingekuwa ni wewe Mfalme ameahidi kwamba endapo utaendelea kumwabudu Mungu aliye hai atakutupa katika tanuru la moto halafu ukaendelea kumwabudu kwa imani kwamba anaweza kukuokoa usitupwe kwenye hilo tanuru, halafu kadri unavyoomba au kanisa linavyoendelea kuomba juu yako huoni kama kuna tumaini la kushinda ungefanyaje? 

SHETANI ANAKULETEA KUWA NA MASHAKA NA MUNGU WAKO NA HATA UNAWEZA UKAONA HILO NENO LA KUWA BWANA NI NGOME KWAKO NI LA UONGO. 

Labda ni kesi inaendelea mahakamani tena ya kusingiziwa halafu bado wiki moja hukumu isomwe.
Kanisa linaomba na kufunga kwaajili yako lakini badala ya ushindi unashangaa unahukumiwa hata kifungo cha maisha. 
Usipokuwa makini hapo shetani anaweza akakuondolea imani yako. 

Yesu anataka uingie mpaka huko gerezani ili akajitwalie utukufu hukohuko. 
Yesu alimwacha mfalme Nebukadreza awatupe kwenye tanuru ili aonyeshe njia pasipokuwa na njia kabisa kwa akili za kibinadamu. 
Shetani asije akakufanya ukafadhaika kwaajili ya ile hatua mbaya ya mwisho inayoonekana kutokuwa na matumaini kabisa kisha akaipora imani yako.

YOHANA 11:3
Basi wale maumbu wakatuma ujumbe kwake wakisema, Bwana, yeye umpendaye hawezi.

****************
Wakati Lazaro akiwa mgonjwa Yesu mponyaji alipata taarifa zake. 
Na zaidi ya yote biblia inamtambulisha kwamba alikuwa ni rafiki yake. 
Rafiki ni mtu wa karibu sana anayeweza kukusaidia kwa dhati kabisa katika changamoto zako. 
Yesu akishakuwa rafiki kwako hakuna kitakachoshindikana tena. 
Unaweza ukawa na tatizo kubwa mno huku ukiwa wewe ni rafiki yake Yesu yani unaishi kwa misingi yote ya neno la Mungu lakini bado ukaomba juu ya jambo lenyewe halafu ukaona hujibiwi chochote. 

Kama Lazaro pamoja na kuwa rafiki yake Yesu na kumtaarifu kuhusu ugonjwa wake lakini Yesu alinyamaza kimya mpaka mauti yakamkuta. 
Sasa hapo shetani aliingiza mawazo mabaya kwa dada zake Lazaro na kuanza kumlaumu Yesu kwamba angekuwepo wala kaka yao asingekufa. 
Imani yao ilianza kuyumbishwa na kuanza kunung'unika na wakati manung'uniko ni dhambi kwa Mungu na ni kama kumuona Yesu kakosea na wakati huwa yeye hakosei. 
Yesu alinyamaza mpaka Lazaro akafa na akazikwa mpaka mwili kuanza kuharibika. 

YOHANA 11:38-44
Basi Yesu, hali akiugua tena nafsini mwake, akafika kwenye kaburi. Nalo lilikuwa ni pango, na jiwe limewekwa juu yake.

Yesu akasema, Liondoeni jiwe. Martha, dada yake yule aliyefariki, akamwambia, Bwana, ananuka sasa; maana amekuwa maiti siku nne.

Yesu akamwambia, Mimi sikukuambia ya kwamba ukiamini utauona utukufu wa Mungu?

Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema, Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia.

Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia sikuzote; lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma.

Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje.

Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake amefungwa leso. Naye Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake.

***************

Yesu alisubiri mpaka siku ya nne maana ilikuwa ni imani ya wayahudi kwamba mtu akifa anaweza akarudi siku ya tatu. 
Walikuwa wanaamini kwamba mtu anapokufa huwa roho yake inakuwa maeneo hayo ikitafuta namna ya kuurudia ule mwili. 
Ndiyo maana Yesu alisubiri mpaka zile siku zao wanazoziamini zipite na waamini kabisa kwamba hapa haiwezekani tena Lazaro kuwa hai kwa namna yoyote ya kibinadamu. 
Yesu anasema kabisa kwamba alifanya hivyo kwaajili ya mkutano ule ili waamini kwamba yeye ni ngome siku ya ile taabu yao. 
Ili waamini kabisa haya yamefanyika kwa Mungu tu na kwa namna ya kibinadamu isingewezekana, BWANA YESU ASIFIWE SANA. 

Sasa usiwe ukawa unamcha Mungu na unapitia katika mambo magumu halafu shetani akaja akakunyang'anya imani yako. 
Endelea kumwamini Mungu. 

UFUNUO 2:9-10
Naijua dhiki yako na umaskini wako, (lakini u tajiri) najua na matukano ya hao wasemao ya kuwa ni Wayahudi, nao sio, bali ni sinagogi la Shetani.

Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.

***************

Mungu anakujuwa na yeye ni ngome wakati wa shida yako, 
Endelea kumwamini kama Lazaro alivyoendelea kuamini mpaka mauti na hata alipokufa kila mtu akajuwa hapa habari ya Lazaro imekwisha lakini pale wanadamu walikoishia Yesu akaanzia pale na utukufu wa Mungu ukaonekana. BWANA YESU ASIFIWE SANA.

Shetani anapokuja kwako wakati wa taabu yako huwa anakuja kukunyang'anya imani yako. 
Anakuja kukudanganya kwamba, 
KAMA KWELI MUNGU NI MWEMA NA NI NGOME SIKU YA TAABU NA HUWAJUWA WAMKIMBILIAO NI KWANINI UNAENDELEA KUWA KATIKA WAKATI MGUMU ZAIDI YA JANA? 

Mbona jana ulikuwa afadhali kuliko Leo? Mbona kadri unavyomkimbilia huyo Mungu ndivyo hali inavyozidi kuwa mbaya zaidi? 
LAKINI SHETANI ANAJUWA KABISA UTAKACHOKIPATA NA ATAKAVYOAIBIKA ENDAPO UTAENDELEA KUMWAMINI MUNGU. 

Anakuletea mawazo mengi mengi yote yaliyo kinyume na Mungu tu. 
Anakuletea mawazo ya kutafakari juu ya haja ya moyo wako na jinsi haja hiyo ilivyo kinyume kabisa na wakati unaopitia. 
Unaugua na unatamani ungekuwa mzima, 
Umesingiziwa kesi na unatamani ungeweza kuaminika unachokiongea kuwa ni kweli. 
Usipokuwa makini unaweza kumwona Mungu ni muongo katika neno lake na ukishaamini hivyo ujue tayari imani yako kwa Mungu imeshakwapuliwa. 

YAKOBO 1:14
Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa.

***************
Tamaa ya mtu ni jambo analoliona la muhimu sana na linachukuwa nafasi ya pili kutoka Mungu. 
Sasa shetani anaweza kuifanya tamaa yako kuchukuwa nafasi ya Mungu katika maisha yako. 
Ukadhiriki kumwacha Mungu kwa ajili ya ile haja kubwa ya moyo wako. 

Shetani akikuona una imani sana na Mungu wako huwa anakuja kukutikisa wakati wa wewe kujaribiwa na ile tamaa yako. 

Palipo na changamoto yoyote kwako Mungu yuko hapo na shetani pia yuko hapo na ni lazima aje hapo tu maani ni kiherehere sana. 

MWANZO 22:1-2
Ikawa baada ya mambo hayo Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa.

Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.

**************
Tamaa ya Ibrahimu ya Muda mrefu ilikuwa ni kumpata mtoto na ndiyo maana hata shetani alimjia na kumpa wazo la kuzaa na Hajiri ambapo shetani alipitia kwa mke wake. 
Isaka alikuwa haja ya Ibrahimu siku zote na Ibrahimu akajaribiwa tena kwa mara nyingine kwa ile tamaa yake ya muda mrefu na haja ya moyo wake ambayo ni Isaka mwanaye. 

Lakini shetani alishindwa kuitikisa Imani ya Ibrahimu na hii ni imani kubwa mno kwani Yule mtoto alikuwa na ahadi nyingi sana na ni kama hazina kubwa sana kwa Ibrahimu. 
Ibrahimu hakujali hilo na ndiyo maana ni baba wa imani. 

MWANZO 22:8-13
Ibrahimu akasema, Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka, mwanangu. Basi wakaendelea wote wawili pamoja.

Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni.

Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe.

Ndipo malaika wa BWANA akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa.

Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee.

Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe.

****************
Ibrahimu alijuwa kabisa kwamba Mungu ni ngome siku ya taabu na ndiyo maana hata Isaka alipomwuliza habari za mwanakondoo alimjibu Mungu atajipatia. 

Mpaka hatua ya mwisho kabisa ambapo Ibrahimu alikuwa amchinje mwanawe na kulikuwa hakuna jinsi nyingine ya kibinadamu Mungu akaanzia pale na utukufu wake ukaonekana, BWANA YESU ASIFIWE SANA. 

SIRI
Mungu hawezi akakubali kuwa ngome kwako wakati wa taabu halafu atokee mtu na miungu yake naye aseme hata hivi alivyofanya Mungu na mimi naweza kufanya na miungu yangu. 
Utukufu wa Mungu hauguswi ni kitu kingine chochote. 

SIFA NA UTUKUFU NI KWAKO MUNGU KWA JINA LA YESU KRISTO. 
NI KWA NEEMA ZAKO TU UMENIFUNULIA HAYA YALIYOSHINDA AKILI NA MAARIFA YOTE YA WANADAMU. 
ASANTE SANA ROHO MTAKATIFU, HAKIKA WEWE NI MWALIMU MWEMA. 
YALELUYA HALELUYA

#Powered_By_Holly_Spirit

No comments:

Post a Comment