Friday, 27 April 2018

NDOA YENU ILIVYO NI MATOKEO YA MATENDO YENU


BWANA YESU ASIFIWE

Leo nakuletea somo lenye kichwa kinachosema, 

NDOA YENU ILIVYO NI MATOKEO YA MATENDO YENU

Roho mtakatifu kanifundisha hilo somo kwaajili ya baadhi ya mambo ambayo huwa tunamlaumu Mungu lakini wala hatustahili. 

Kila tunachotaka kukifanya huwa tuna mwongozo mzuri sana katika neno la Mungu, 

Na kama tukiufuata huo mwongozo ni lazima tutashinda kwa jina la Yesu Kristo. 

Twende kwenye neno la msingi wa mafundisho yetu. 

ISAYA 48:18

Laiti ungalisikiliza amri zangu! Ndipo amani yako ingalikuwa kama mto wa maji, na haki yako kama mawimbi ya bahari;

*******************

Ukimsikiliza Mungu daima utakuwa mwenye amani juu ya kila majibu ya kila utakachofanya kwasababu utaanza na Mungu na utamaliza na Mungu.

Kamwe hutadhulumiwa haki yako ikiwa unasikiliza amri za Mungu na kutii. 

MFANO

Ni kawaida sana kusikia baadhi ya wanandoa waliooana na kuishi pamoja wakisema kwamba maisha yao yalibadilika na kupoteza amani yote baada tu ya kufunga ndoa.

Hapo utamsikia kila mmoja akimlaumu mwenzake kwamba alikuwa anaficha makucha lakini ukifuatilia maisha yao utagundua siyo kweli na wamefikia hapo walipo kwasababu walimwacha Mungu aliyethibitisha hiyo ndoa. 

Tunaposema wameoana maana yake ni kuendana au kuwa kama sare hiyo ndiyo tafsiri ya kuoana. 

Wale mafundi ujenzi watanielewa nachomaanisha hapa. 

Kama ukikata mbao mwishoni kwa mfano wa herufi "Z" au kimshazari ni lazima mbao nyingine ukate kama hiyo ili zioane utakapounganisha. 

MWANZO 2:18

BWANA Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.

**************

Ndiyo maana hata Bwana Mungu alilijuwa hilo akamfanyia Adamu wa kufanana naye. 

Kufanana kunakoongelewa hapa siyo sura, umbo au rangi la! 

Kufanana kunakoongelewa hapa ni katika mambo yote. 

Kama uliyenaye hamjafanana na kuoana hamtaoana hata katika tendo la ndoa. 

Kama hamjafanana(hamjaoana) hata mtakapofanya tendo la ndoa mtashangaa mwanamke anakuwa na maumbile madogo na mwanaume maumbile makubwa au mwanaume yanakuwa makubwa na mwanamke madogo mnaishia kuumizana kila siku. 

Hamtaoana hata katika starehe zenu za kawaida. 

AMOSI 3:3

Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana?

****************

Wewe utataka kwenda kaskazini na yeye atataka kwenda kusini kwasababu hamjaoana. 

Yani kila mtakachopanga hamtaweza kuoana katika mawazo yenu. 

Mjue hapo yupo ambaye ameshaenda kinyume na yale makubaliano na viapo mlivyoapa pale madhabahuni

Yupo ambaye hajasikiliza amri za Mungu akafungua mlango adui akaingia.

Ndiyo maana amani hakuna, wala haki yako haitakuwepo.

Ulichopaswa kupewa na mume wako utakitafuta wewe na pia huyo mume naye atakuwa anapata haki yake kwa shetani.

Yani ndiyo pale mwanamke anapofika hatua ya kumkomoa mume wake kwa kumnyima tendo la ndoa ambayo ni haki yake kabisa. 

Mwanaume ataamua kuitafuta hiyo haki kwa Mwanamke mwingine na hapo ndipo tunaposema kuwa ameipata kwa shetani. 

Baraka hazitakuwepo. 

KIAPO

Katika kiapo chochote unachomtaja Mungu lazima Mungu ashuke awepo kuthibitisha. 

MALAKI 2:14
Lakini ninyi mwasema, Ni kwa sababu gani? Ni kwa sababu BWANA amekuwa shahidi kati ya wewe na mke wa ujana wako, uliyemtenda mambo ya hiana, angawa yeye ni mwenzako, na mke wa agano lako.

**************

Sasa usifanye mchezo kabisa katika jambo ambalo Mungu amekuwa shahidi na akaja kuthibitisha maneno yenu mliyoyatamka kwa makubaliano/maagano. 

MWANZO 25:33-34

Yakobo akamwambia, Uniapie kwanza. Naye akamwapia, akamwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza.

Yakobo akampa Esau mkate na chakula cha dengu, naye akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo Esau akaidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.

*****************

Hapa Yakobo anamwambia Esau amwapie kwanza maana alijuwa kabisa kwenye kiapo lazima Mungu wa baba yao wanayemwabudu atashuka kuthibitisha. 

Esau aliondoka akadhani ni kawaida kama vile wanandoa wanavyofunga ndoa wanapanda Madhabahuni mahali patakatifu kisha wanaapa mbele za Mungu kwamba tutakuwa waaminifu, na kupendana halafu baadae uaminifu unavunjwa na mmoja. 

ANGALIA KILICHOMTOKEA ESAU

MWANZO 27:19-29

19 Yakobo akamwambia babaye, Mimi ni Esau, mzaliwa wako wa kwanza, nimefanya kama ulivyoniambia. Ondoka, tafadhali, ukae kitako, ule mawindo yangu, ili roho yako inibariki.

20 Isaka akamwuliza mwanawe, Imekuwaje umepata upesi namna hii, mwanangu? Akasema, Kwa sababu BWANA, Mungu wako, amenifanikisha.

21 Isaka akamwambia Yakobo, Karibu, tafadhali, ili nikupapase, mwanangu, nione kwamba wewe ndiwe mwanangu Esau, ama siyo.

22 Basi Yakobo akamkaribia Isaka, babaye, naye akampapasa, akasema, Sauti ni sauti ya Yakobo, lakini mikono ni mikono ya Esau.

23 Wala hakumtambua, kwa maana mikono yake ilikuwa kama mikono ya Esau, ndugu yake, yenye malaika; basi akambariki.

24 Akamwuliza, Wewe ndiwe kweli mwanangu Esau? Akasema, Ndimi.

25 Akasema, Niletee karibu nami nipate kula mawindo ya mwanangu, ili roho yangu ikubariki. Akamsogezea karibu, naye akala; kisha akamletea mvinyo, akanywa.

26 Isaka, baba yake, akamwambia, Njoo karibu sasa, ukanibusu, mwanangu.

27 Akakaribia akambusu. Naye akasikia harufu ya mavazi yake, akambariki akasema,Tazama, harufu ya mwananguNi kama harufu ya shamba alilolibariki Bwana.

28 Mungu na akupe ya umande wa mbingu,Na ya manono ya nchi,Na wingi wa nafaka na mvinyo.

29 Mataifa na wakutumikieNa makabila wakusujudie,Uwe bwana wa ndugu zako,Na wana wa mama yako na wakusujudie.Atakayekulaani alaaniwe,Na atakayekubariki abarikiwe.

*******************

Unaweza ukafikiri Rebeka na Yakobo walifanya hizi hila au utapeli huu kwa namna ya kawaida lakini ni mpango wa Mungu kabisa na Mungu alitetea haki ya Yakobo kwasababu alikumbuka siku waliyoapa kwa jina lake.

KWANINI MASURIA WENGI WANAISHI KWA AMANI TOFAUTI NA WANANDOA? 

Ni rahisi sana kusikia wanandoa wakilalamika kila mmoja akimlaumu mwenzie kwamba walipokuwa wakiishi pamoja bila ndoa mambo hayakuwa mabaya kama wanavyoishi baada ya kuhalalisha mahusiano yao kwa Mungu kwa njia ya kiapo madhabahuni. 

YOHANA 8:47

Yeye aliye wa Mungu huyasikia maneno ya Mungu; hivyo ninyi hamsikii kwa sababu ninyi si wa Mungu.

***************

Ili mahusiano yoyote ya wanaopendana kwa lengo la kuoana au ya watu wanaoishi pamoja yawe na kibali mbele za Mungu ni lazima myapeleke mbele zake. 

Kama hamjayapeleka mbele za Mungu basi mjue hamjamsikiliza Mungu hivyo ninyi siyo wa Mungu. 

Na kama ninyi si wa Mungu basi ni wa shetani. 

ISAYA 1:19-20

Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi;

bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha BWANA kimenena haya.

****************

Ili mle mema ya nchi kama asemavyo Bwana Mungu ni lazima utii maagizo yake yote aliyoagiza mtekeleze mkiwa wana ndoa mliooana. 

Lakini pia msipomtii Mungu na kusikiliza maagizo yake utakuwa kinyume naye na hapo mtakuwa wa shetani. 

Hivyo mkimtii shetani na kumsikiliza mtakula mema yake ya dunia ambayo ni uharibifu na ni lazima dunia itawanyoosha tu. 

Mema ya shetani mtakayokula ni kama yafuatayo. 

Kama mnaishi miaka yote bila ndoa mtaona kama mna amani ndani yenu kumbe siyo amani bali ni shetani kawatengenezea amani ya uongo. Hakuna amani hapo maana hayo maisha yenu Mungu hajayapa kibali hivyo yameshikiliwa na shetani ambaye katika ufalme wake hana kitu kinachoitwa amani. 

Amani ipo kwa Yesu Kristo tu na ndiye mfalme wa amani. 

Hiyo mnayodhani ni amani mwisho wake ni lazima iwe kilio. 

METHALI 14:12

Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu,Lakini mwisho wake ni njia za mauti.

***************

Shetani anawabembeleza na mnakula mema yake na tena anawajibika ipasavyo maana mmemtii yeye. 

Anapenda sana usaliti na mmoja wenu kuvunja makubaliano mliyowekeana. 

Mmoja akimsaliti mwenzake shetani anajitahidi kumficha huyo mwingine asione ili mzidi kuaminiana na baadaye mfunge ndoa hata kama hamjaoana(hamjafanana) ili tu aharibu lile kusudi la Mungu kwamba

 "akamfanyia msaidizi wa kufanana naye"

Mungu anafunua siri zote lakini shetani hafunui siri.

Yani mlivyokubali kumtii mkaishi bila kufunga ndoa kama atakavyo yeye ataficha maovu ya kila mmoja na siri zake mbaya na chafu ili mridhishane na kujiona waaminifu tena mnaoendana.

Kumbe hamfanani wala hamuoani. 

Ingekuwa nyinyi ni wanandoa mliokula viapo kwamba mtakuwa waaminifu halafu mmoja wenu akatoka nje ni lazima Mungu angefunua hiyo siri kwa mwenzake maana Mungu hafichi uovu. 

LUKA 8:17

Kwa maana hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa ambalo halitajulikana na kutokea wazi.

*****************

Hakuna uovu unaofichwa na Mungu ikiwa mlimkabithi mahusiano yenu ayalinde. 

DANIELI 2:22

Yeye hufunua mambo ya fumbo na ya siri; huyajua yaliyo gizani, na nuru hukaa kwake.

*****************

Kama Nuru hukaa kwa Mungu na kweli yote basi ujue giza hukaa kwa shetani na yeye ndiye baba wa uongo. 

Kwahiyo mkishafunga ndoa mtahisi kwamba hayo mambo ni mapya lakini siyo mapya ila yalikuwepo tangu mwanzo na ni shetani alikuwa ameyaficha katika giza lakini sasa kwakuwa mmempa Mungu nafasi yeye anayaweka katika nuru. 

NDOA KAMILI

Mnapofunga ndoa na kula kiapo mbele ya madhabahu ya Mungu mjue kabisa mmoja wenu atakapokiuka kile kiapo ni lazima moto uwake tu. 

Esau alitaka kukiuka kile kiapo lakini Mungu akasema na Rebeka akamwambia haiwezekani maana kuna kitu walishakubaliana tena wakaniita nikathibitisha. 

Mungu hapotezi kumbukumbu. 

Mnakula kiapo kwamba 

"MTAPENDANA KATIKA SHIDA NA RAHA"

"MTAKUWA WAAMINIFU"

Mnapotamka hivyo tu Mungu anagonga mhuri na atakuwa anakiangalia kile kiapo chenu kila siku. 

Kwakuwa mmempa Mungu hilo jukumu la kuwalinda na mkajileta mbele zake basi atawalinda na mtakuwa mnapendana kweli kwakuwa mnamcha BWANA. 

Nasema mtakuwa mnapendana kwakuwa mnamcha BWANA kwasababu. 

KAMA HAKUNA NGUVU YA MUNGU NDANI YAKO HUWEZI KUWA NA UPENDO WA KUJIPENDA WEWE MWENYEWE WALA KUMPENDA MTU MWINGINE. 

Ndiyo maana unakuta mtu ni 

Mlevi, mzinzi, anaendesha gari kwa kasi, anaharibu ngozi yake kwa kujichubua, teja, haogi, anajitesa na njaa bila sababu, nguvu zake zote na jasho lake wanafaidi malaya. 

HUKO KOTE NI KUTOKUJIPENDA NA KUTOKUJUWA THAMANI YAKO. 

Sasa mtu mwenye tabia moja kati ya hizo atasemaje anampenda mtu mwingine ikiwa kujipenda yeye tu ameshindwa? 

Kumpenda mtu mwingine ni neema ya Mungu ila pasipo hiyo neema huwezi kujipenda hata wewe mwenyewe. 

Hivyo usije ukawaona watu wanaishi kwenye mahusiano kinyume na neno la Mungu ukafikiri wanapendana hamna upendo hapo bali ni uongo wa shetani tu. 

Neno linasema kabisa

YOHANA 8:47

Yeye aliye wa Mungu huyasikia maneno ya Mungu; hivyo ninyi hamsikii kwa sababu ninyi si wa Mungu.

******************

Nyinyi siyo wa Mungu mmepata wapi huo upendo? 

Kwani shetani alisema tupendane? 

Mungu atakavyoilinda ndoa aliyoithibitisha na wanandoa wakajiheshimu na kuheshimu kile kiapo huwa shetani anaugua kabisa.

Akiwaona mnaishi kwa msingi wa kile kiapo huwa anakuja kuwajaribu kama kweli mtaendelea kushinda. 

Mtakapoishi kwa misingi ya kile kiapo yani mnapendana na kuwa WAAMINIFU hapo Mungu anaachia baraka zake zinakuja na mtafanikiwa na kuishi kwa furaha maisha yenu yote. 

Shetani anapokuja ili awatikise ili kupima misimamo ya imani yenu huwa anaangalia mlango wa kupitia kwakuwa nyie mmezungushiwa wigo.

YAKOBO 1:14-15

Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa.

Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.

***************

Adui akija kwenu wanandoa anakuta mmezungukwa na ulinzi wa Mungu, lakini anachunguza mioyo yenu je, ni yupi naweza kumwingia ili niharibu nyumba nzima? 

Kuna mtu unakuwa umesimama na Mungu lakini kuna kitu fulani huwa ndicho kimekuwa dhambi ya mara kwa mara kwako japo unatubu na kusamehewa lakini unajikuta umerudia tena na tena. 

HIYO NDIYO TAMAA YAKE MTU HUYO. 

Sasa adui anaangalia je wewe baba tamaa YAKO iko wapi au wewe mama tamaa YAKO iko wapi? 

Kama ni kwenye pesa anakukutanisha na mwanaume mwingine mwenye pesa ya kuweza kukushawishi mpaka uzini ili hiyo tamaa ibebe mimba na ikishakomaa izae mauti ya ndoa YAKO. 

Akija kwako baba anaangalia unapenda kitu gani, kama ni wanawake weupe shetani anakupa mzungu kabisa ili uzini na hiyo tamaa ibebe mimba kisha izae mauti ya ndoa YAKO. 

Mnabaki mkijiuliza ni kwanini haya mambo zamani hayakuwepo? Haya mambo yalikuwepo lakini yalijificha kwenye lile giza na uongo wa shetani kwakuwa mlikuwa mnamtii tofauti na sasa ambapo mahusiano yenu YAKO katika ufalme wenye nuru na usioficha maovu. 

Wanandoa mkiishi kinyume na neno la Mungu mtaangamia tu hata iweje. Mungu anafuatilia sana kile kiapo na mtakapokiuka tu mtaangamia. 

Kuna baadhi ya mambo ambayo yakishatokea katika ndoa huwa Mungu anachukizwa nayo sana kiasi cha kugeuka laana katika ndoa na hapo mizozo huanza. 

1PETRO 3:8-9

Neno la mwisho ni hili; mwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitikivu, wanyenyekevu;

Watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi baraka.

*******************

Wanandoa mtakapofanya hayo yote ndipo Mungu atawabariki na mtakula mema ya nchi. 

Lakini mkiacha kushika hata moja kati ya hayo basi mjue kinyume na baraka ni laana iko mbele yenu. 

Mmoja wenu anapofanya jambo tofauti ni adui kapata nafasi ya kuingia ndani lakini bado hajapata nafasi ya kutawala. 

Ili asipate nafasi ya kutawala inatakiwa sasa huyu aliyetendewa aangalie je neno la Mungu linasemaje kwa hili nililofanyiwa? 

WAKOLOSAI 3:12-15

Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu,

mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.

Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu.

Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani.

****************

Neno la Mungu linasema amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu, na ukiwa na amani ya Kristo ni lazima msameheane, siyo kulipa baya kwa baya bali uushinde ubaya kwa wema. 

UNAPOONA MMOJA WENU AMEFANYA JAMBO LILILO CHUKIZO KWA MWENZAKE BASI UJUE HUYO NI SHETANI KAMWINGIA.

HIVYO ILI UMSHINDE SHETANI UNATAKIWA UTUMIE NGUVU ZA MUNGU AMBAZO ZIKO KATIKA NENO LAKE AMBALO LINASEMA TUSAMEHEANE WALA TUSILAUMIANE. 

Lakini ukisema umshinde shetani kwa kutumia neno la shetani ni lazima dhambi itatawala, shetani atatawala na mwisho ni mauti ya ndoa.

HAYA NDIYO MAKOSA

YEREMIA 31:22

Hata lini utatanga-tanga, Ee binti mwenye kuasi? Kwa maana BWANA ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanamume. 

******************

Mwanamke umeambiwa umlinde Mume wako lakini siyo kwa namna ambayo wanandoa wanalindana kwa sasa kwa kuwindana. 

Yani wanandoa wanaishi wakiwindana na kila mmoja anawaza namna ya kujionyesha kwamba yeye ni mwamba kuliko mwenzake. 

Hayo mashindano ya kuwekeana visasi kiasi hicho Mungu hayafurahii kabisa lazima laana itatawala ndani ya nyumba kwasababu mnaishi nje kabisa ya neno lake.

WAEFESO 5:22-25

Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu.

Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili.

Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo.

Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake;

******************

Huwa nikisoma kifungu hiki cha maandiko matakatifu ambayo ni sauti ya Mungu halafu nikiangalia namja ambavyo baadhi ya wanawake wanavyojitahidi kutafuta namna ya kuwa juu ya waume zao ni laana tupu ndiyo maana hata hizi baraka alizoahidi Mungu hazipo kabisa

Nimefanya utafiti maana wapo watu wamenifuata mara nyingi kuniuliza juu ya mahusiano yao yanavyoleta changamoto, pia nikajaribu kuwasikiliza wanawake wanasemaje na wanaume wanasemaje nikapata mawaza tofauti lakini nimegundua kwamba kwa asilimia kubwa hawajajuwa jambo moja tu. 

WAEBRANIA 13:4

Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu. 

******************

Ndoa inahitaji heshima ya kipekee sana na pia kujitambua baina ya wanandoa na majirani na wao kwa wao pia kujitambua kwamba sisi ni watu waliooana. 

Ipo tabia ya zamani ambayo ulikuwa nayo ambayo ni ya kawaida sana ila siyo kwenye ndoa.

Ndoa inahitaji heshima zote.

Tabia zisizooana na tabia za huyo uliyeoana naye achana nazo zitaleta mauti ya ndoa yenu.

Mungu ameshasema ataachilia adhabu endapo utazini na neno la Mungu halipiti bali ni lazima litatimiza mapenzi yake alilolituma. 

Wapo marafiki mnaotakiwa kabisa kuwapa wigo wa mawasiliano yenu, matumizi ya simu zenu ni lazima yawe tofauti na zamani, utani na mazoea na watu wa jinsia tofauti ni lazima msitishe kwani mizaha ni dhambi mbele za Mungu. 

Lazima mwanamke awe chini ya Mwanaume na awe mtii.

Kuwa mtii maana yake ni kutii kila kitu siyo mwanamke kuwa na kiburi.

Kwakuwa wote mpo ndani ya Kristo Yesu wala hakuna haja ya kutomtii mume wako kwa kila kitu kwa kuwa atakayokuelekeza yote yanatoka katika Kristo. 

Kama wewe kijana umeoa na maisha YAKO unayoishi huna tofauti na mtu asiyeoa basi ujue ni lazima dunia ikucharaze tu. 

Kama wewe dada umeolewa na maisha YAKO unayoishi huna tofauti na mtu asiyeolewa basi ujue ni lazima dunia ikucharaze tu. 

Hakuna hila kwa Mungu. 

Utii unapokosekana ndani ya nyumba basi hakuna kitakachoendelea. 

WAFILIPI 2:8

Tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.

********************

Utii unaoongelewa hapa ni utii haswa ikiwa mpo ndani ya Kristo. 

Mwanamke unapotaka kumtawala mume wako au mume unapoacha kumpenda mke wako basi mjue kuanzia hapo mnatembea kwenye laana. 

Kama kila mmoja akisoma neno na kusimama kwenye nafasi yake kama biblia inavyomuelekeza wala hakuna kitakachopungua. 

Siri ya kushinda majaribu ya ndoa siyo uzuri na urembo wa mke au familia kuwa matajiri bali siri iko katika kuishi ndani ya neno. 

METHALI 31:30

Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili;Bali mwanamke amchaye BWANA, ndiye atakayesifiwa.

******************

Mwanamke anayesimama na Mungu ni lazima mume wake amsifu na pia mwanaume anayesimama na Mungu ni lazima mke wake amfurahie. 

Wasichana na vijana wote wa sasa wametekwa na dunia.

Sasa ni bora usijue vitu vyote lakini ujue tu hiki kitakusaidia sana katika maisha yako yote,  kwamba

METHALI 19:14

Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye;Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na BWANA.

******************

Hata kama huyo mke mwema utapewa au mume mwema utapewa na Bwana lakini mkashindwa kuishi kwa kusoma neno basi ni lazima mtaishi kwa kubahatisha tu maana msingi wa wanandoa kuishi ni ni kwa neema ya Mungu na ndiyo maana neno linasema

METHALI 31:30

Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili;Bali mwanamke amchaye BWANA, ndiye atakayesifiwa.

********************

Mwanamke amchaye BWANA ndiye atakayesifiwa kwakuwa atakapomcha BWANA ni lazima ataishi na mume wake kwa mwongozo wa neno la Mungu linavyotaka. 

Kila jambo mwezako analokufanyia wewe angalia neno la Mungu linakuelekeza kufanya nini halafu fanya. 

Kama ni kuomba wewe omba na uwe mwaminifu kwa Mungu ni lazima yeye atakutetea. 

Atakufunulia siri usizoamini. 

Lakini cha kushangaza wanandoa wanatumia akili zao wenyewe na wakati ndoa wanayoishi ndani yake ni Mungu aliwapa. 

Tumia akili zako lakini usizitegemee hata kidogo. 

METHALI 3:4-6

Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri,Mbele za Mungu na mbele ya mwanadamu.

Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote,Wala usizitegemee akili zako mwenyewe;

Katika njia zako zote mkiri yeye,Naye atayanyosha mapito yako.

*******************

Ukimtegemea Mungu ni lazima utawapendeza wanadamu na mbele za Mungu. 

Wanadamu watawasifu na kila mtu atatamani maisha yenu. 

Mtafurahiana na neema ya upendo kwenu itaongezeka pia kila siku itakuwa mpya kwenu na yenye mafanikio makubwa kiroho na kimwili. 

METHALI 31:28-29

Wanawe huondoka na kumwita heri;Mumewe naye humsifu, na kusema,

Binti za watu wengi wamefanya mema,Lakini wewe umewapita wote.

******************

ASANTE SANA ROHO MTAKATIFU MAANA WEWE NI MWALIMU MWEMA. 

SIFA NA UTUKUFU NI KWAKO YESU KRISTO. 

#Powered_By_Holly_Spirit

No comments:

Post a Comment