Friday 27 April 2018

YESU KRISTO NI YEYE YULE JANA NA LEO NA HATA MILELE.


BWANA YESU ASIFIWE

Leo nakuletea somo lenye kichwa kinachosema, 

YESU KRISTO NI YEYE YULE JANA NA LEO NA HATA MILELE. 

Leo Roho Mtakatifu amekusudia kutufundisha namna ambavyo YESU Kristo alivyo ukomboa huu ulimwengu tangu mwanzo na namna anavyoendelea kuyapigania maisha yetu.
Kuhakikisha kwamba mwanadamu anakuwa huru. 
Hakika sifa na utukufu na heshima na mamlaka vyote ni vya kwake. 

TWENDE KWENYE NENO LETU LA MSINGI

WAEBRANIA 13:8
Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele.

**************
Wapo watu wanakuwa na uelewa mdogo kuhusu AGANO LA KALE na AGANO JIPYA kuhusu YESU KRISTO. 
YESU KRISTO hajakuwako katika AGANO JIPYA peke yake. 
Alikuwepo katika MAAGANO yote makubwa mawili.
Bali alijithihirisha waziwazi katika AGANO JIPYA. 

MWANZO 3:21
BWANA Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika.

**************
Baada ya Adamu kufanya dhambi kwa kula lile tunda ambalo Mungu alimkataza hawakuweza tena kumkaribia Mungu kwaajili ya dhambi hiyo. 
Na pia Mungu hakuweza kuwakaribia kwaajili ya dhambi iliyokuwa mbele yao ya kuwa wa uchi. 

Bwana Mungu aliwafanyia mpango wa kufunika uchi wao ambapo ili kulifanikisha hilo ilibidi Bwana Mungu awafanyie mavazi ya ngozi. 

Tafsiri ya ngozi nyuma yake lazima kuwe na mauti, 
Na nyuma ya mauti lazima kuwepo na kumwaga damu. 
Kuna usemi wa sasa wanasema 
"ukiona manyoya ujue kaliwa. "
Au aliyekamatwa na ngozi ndiye mwizi.
Kwa hiyo hapa tunaona kabisa kwamba, ili mwanadamu huyu aliyetenda dhambi aweze kumkaribia tena Mungu ni lazima damu imwagike. 
Ile damu ya yule mnyama aliyechinjwa na Mungu mwenyewe ndiyo iliyoweza kumkomboa mwanadamu kutoka katika dhambi aliyoifanya. 

WAEBRANIA 10:1-10
Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao.

Kama ndivyo, je! Dhabihu hazingekoma kutolewa; kwa maana waabuduo, wakiisha kusafishwa mara moja, wasingejiona tena kuwa na dhambi?

Lakini katika dhabihu hizo liko kumbukumbu la dhambi kila mwaka.

Maana haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi.

Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema,Dhabihu na toleo hukutaka,Lakini mwili uliniwekea tayari;

Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo;

Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa)Niyafanye mapenzi yako, Mungu.

Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati),

Ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili.

Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.

******************
Katika nyakati hizo mwanadamu aliendelea kutakaswa kwa damu ya mafahali na mbuzi, 
Yote hayo yalifanyika lakini Mungu akiyatambua kwamba ni kama kivuli tu cha mambo halisi yajayo. 
Pamoja na Mungu kuchaguwa kwamba njia ya mwanadamu kumwendea anapokuwa na dhambi ni lazima atumie damu lakini ile damu ya wanyama bado aliona kuwa haitoshi kumfanya atakasike na kuwa tayari kuuona uso wa Mungu.
Ndiyo maana Yesu alikuja akaliondoa lile AGANO akasimamisha la kwake ambalo ni la damu isiyo na mawaa, damu isiyoguswa na chochote. 

Mtoto anapokuwa tumboni huwa na damu yake mwenyewe wala damu ya mama haihusiki kivyovyote na damu ya mtoto. 
Damu ya mtoto ni ya mtoto na baba yake, na damu ya mama ni ya mama peke yake.
Ndiyo maana pia mimba ya Maria haikuwa na baba. 
Kama ingekuwa na baba basi Yesu angekuwa na damu yenye uhusiano na damu ya mwanadamu wa kawaida. 
Yesu alizaliwa kama mwanadamu, na kila kitu alifanya kama mwanadamu lakini hakutokana na kizazi cha mwanadamu. 
HIYO NDIYO TOFAUTI KATI YA YESU NA MWANADAMU. 

Wakati wa AGANO LA KALE Yesu alikuwa akijitokeza sehemu mbalimbali kwa kivuli cha damu yake kuokoa, kutakasa na hata kuponya. 

HESABU 21:6-9
BWANA akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa.

Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung’unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa BWANA, atuondolee nyoka hawa. Basi Musa akawaombea watu.

Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi.

Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.

********************
Hapa tena Yesu alijitokeza kwa sura ambayo hawakuielewa. 
Kwanini Mungu amwambie Musa amtundike huyo nyoka wa shaba? 
Na kweli kila aliyeumwa na nyoka alipoinua macho kumtazama basi aliishi, lakini wapo waliokataa kabisa kumtazama na walikufa. 

YOHANA 3:14-15
Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa;

Ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye.

********************
Leo hii wapo watu wenye matatizo na wanaendelea kung'ang'ana dini zao lakini hawamtaki Yesu kabisa wala hawataki kusikia habari ya kuokoka na wanakufa na matitizo ambayo endapo wangekubali kuinua macho juu na kumtazama Yesu pale msalabani wangepona kabisa. 
Mwana wa Adamu aliinuliwa pale msalabani ili kila atakayemwamini na kuinua macho kumtazama awe na uzima wa milele. 

Yesu anaokoa, Yesu anaponya na pia huwafanya watu kuwa huru. 

KUTOKA 12:11-14
Tena mtamla hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya BWANA.

Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi BWANA.

Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri.

Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa BWANA; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele

******************
Wana wa Israeli walikaa utumwani miaka yote mia nne bila ukombozi wa aina yoyote. 
Tena Musa alivyotumwa na Mungu Farao alikuwa mbishi kuwaachia watu wake. 
Mungu aliipiga Misri kwa mapigo tisa lakini yote yale hayakusaidia wana wa Israeli kuwa huru. 
Kwa mapigo yote tisa hawakujikomboa, hawakupata kuwa huru wala hawakuokoka. 
Lakini hili pigo la kumi ndilo pigo ambalo Yesu Kristo alijitokeza katika sura ya damu na kwa kupitia hiyo damu waliachiwa huru. 
Ishara yoyote katika biblia iliyokuwa na sura ya damu ndani yake kwaajili ya uponyaji, uokoaji au kuweka watu huru ilibeba picha ya Yesu Kristo. 
Kwa kuwa Farao alimshikilia mzaliwa wa kwanza wa Mungu kama alivyomtaja basi Mungu akaachilia mapigo kwa wazaliwa wote wa kwanza wa kila mnyama na mwanadamu katika Misri.
Hakuna nyumba iliyokuwa haina msiba siku hiyo wala hakukuwa na wa kumfariji mwenzie. 
Kwa ile damu wana wa Israeli waliyoipaka kwenye milango ndiyo iliyowakomboa. 
Hapo ndipo ilipoanza PASAKA (PASSOVER) 
Mungu akimaanisha kwamba ata passover (atapita juu) yao atakapoiona ile damu kwenye miimo ya milango yao. 
Na Mungu akaagiza iwe kumbukumbu si sikukuu vizazi vyote.

Tangu wakati wa AGANO LA KALE Yesu aliendelea kufanya ishara na maajabu makubwa kwaajili ya kuwakomboa watu kutoka kwenye utawala wa shetani ibilisi. 

1YOHANE 3:8
Atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.

**************
Ibilisi alitenda dhambi tangu mwanzo akiwa hapa ulimwenguni. 
Tangu mwanzo alitenda dhambi kwa kumdanganya HAWA ale lile tunda. 
Mwanadamu akaanza kutawaliwa na dhambi. 
Lakini kwa ile damu iliyomwagika ili kupatikana ngozi ya kumvika mwanadamu kuuficha uchi wake inaonyesha kabisa hata Yesu alikuwa anatenda kazi tangu mwanzo. 
Ila tu hakuwa amedhihirishwa. 
Katika AGANO JIPYA biblia inatuambia, 
"Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za ibilisi."
Hatutakuwa tena wa ibilisi ikiwa amedhihirika kwetu. 

WAEBRANIA 9:15-17
Na kwa sababu hii ni mjumbe wa agano jipya, ili, mauti ikiisha kufanyika kwa kukomboa makosa yaliyokuwa chini ya agano la kwanza, hao walioitwa waipokee ahadi ya urithi wa milele.

Maana agano la urithi lilipo, lazima iwepo mauti yake aliyelifanya.

Kwa maana agano la urithi lina nguvu palipotukia kufa kwa mtu; kwa kuwa halina nguvu kabisa, akiwa yu hai yeye aliyelifanya.

********************
Mauti yake ilifanyika ili tuwe tunatakasiki kwa namna nyingine kabisa ya neema inayodumu. 
Na ilikuwa ni lazima afe ili hilo AGANO JIPYA la damu alilolileta liweze kuwa na nguvu. 
Kama mtu hujafa hata barua za mirathi ulizoziandika kwaajili ya watoto kwamba huyu atarithi hiki na yule atarithi kile hazitaweza kusomwa. 
Siku mtu akifa ndipo zile barua zitakapokuwa na thamani tena kubwa sana. 
Huwezi kusikia kuna kesi ya mirathi mahakamani ikiwa yeye aliye mmiliki wa ile mirathi hajafa. 
Hivyo Yesu alikufa ili hili AGANO JIPYA la damu liwe imara. 

WAKOLOSAI 1:13-17
Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake;

Ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi;

Naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.

Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake.

Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye.

****************
Alikuja na kudhihirika kwetu kwaajili tu ya msamaha wa dhambi, kumkomboa mwanadamu. 
Na biblia inatuambia kwamba alikuwako kabla ya vitu vyote. 

Katika ile siku ambayo wana wa Israeli waliambiwa kuwa wapake ile damu kwenye miimo ya milango ili wasipate pigo la kuondokewa mzaliwa wa kwanza kwao, ile damu ilikuwa ni kivuli cha damu ya Yesu na ndiyo maana baada ya Yesu kudhihirika kwetu alikuja kujionyesha kwamba ni yeye kwenye kumbukumbu na sikukuu ambayo Mungu aliwaambia waifanya kwa vizazi vyote. 

LUKA 22:19-20
Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.

Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.]

*****************
Kama vile wana wa Israeli walivyoambiwa waikumbuke hiyo siku ya pasaka vizazi vyote, 
Ndiyo hivyo hivyo Yesu alivyojidhihirisha katika siku hiyo na kutuambia pia tuendeleze hiyo kumbukumbu. 
Kufa kwake na kufufuka kwake kuliikamilisha maana halisi ya pasaka na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. 

Sasa tunao ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu. 

LUKA 23:44-46
Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda,

Jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati.

Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.

*******************
Tulikuwa hatuwezi kuingia kwenye pazia la hekalu ili tukatubu dhambi zetu bila damu lakini kwaajili ya pasaka maana kile kifo chake ni kikombe cha AGANO JIPYA katika damu yake. 

WAEFESO 6:3-8
Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake?

Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.

Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake;

Mkijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena;

Kwa kuwa yeye aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi.

Lakini tukiwa tulikufa pamoja na Kristo, twaamini ya kuwa tutaishi pamoja naye;

********************
Tunaweza kuitumia ile damu ya Yesu ikiwa tumetii yote aliyotuagiza, 
Tuliobatizwa katika Kristo Yesu ndiyo tuliokubali kufa naye katika mauti yake na kufufuka naye. 
Wala sisi siyo wafu tena kwaajili ya dhambi ikiwa tumetii yote. 
Yesu anatawala na tunatawala naye kwani kwa njia ya wokovu na ubatizo tulimkiri tukaunganika nanye katika mauti yake, tukafufuka naye na sasa tunatawala naye. 

LUKA 24:47
Na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu.

********************
Yesu Kristo habagui wa kumtakasa, yeyote aliyekubali kumpokea na kufuata njia zake huyo ndiye wa kwake. 
Na ameahidi kuwa yeyote aliyelishika neno lake huyo ndiye wakwake na kamwe hatamwacha. 

MATHAYO 28:18-20
Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.

Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu;

Na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.

****************
Yesu anataka uyashike yote aliyotufundisha, lakini siyo uamini na kufuata baadhi ya maandiko lakini mengine uyapuuze. 
Mafundisho ya dini za wanadamu na mapokeo yake yasikufanye ukapuuza neno na mafundisho ya kweli ya Kristo Yesu. 
Yeye yuko na sisi mpaka ukamilifu wa dahari. 


ASANTE SANA ROHO MTAKATIFU MAANA WEWE NI MWALIMU MWEMA. 

#Powered_By_Holly_Spirit.

No comments:

Post a Comment