Thursday 10 May 2018

NGUVU YA KUISHINDA DHAMBI NA MATENDO YOTE MABAYA.

BWANA YESU ASIFIWE NA KUPEWA UTUKUFU WOTE.

Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu Leo tunajifunza somo lenye kichwa kinachosema,

NGUVU YA KUISHINDA DHAMBI NA MATENDO YOTE MABAYA.

Kwa sisi wateule wa Mungu tulionunuliwa kwa damu ya Yesu Kristo tena damu ya thamani huwa tunaugua sana tunapojikuta tumeanguka katika dhambi.
Lakini leo Roho Mtakatifu yuko hapa na sisi kwa ajili ya kutusaidia katika madhaifu yetu.
BWANA YESU ASIFIWE SANA.

Neno la msingi katika mafundisho yetu.

METHALI 4:23
Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo;Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.

*************
Moyo ndiyo kitu cha kulinda sana kuliko vitu vyote maana uzima uko ndani yake.
Moyo unapoharibika basi utakuwa huna tena uzima ndani yako.
Chemchemi za uzima ni ule uwezo wa kutenda mema tu.
Maana katika msamaha wa dhambi kuna nguvu ya uponyaji ndani yake.
Yesu anasema kuwa alikuja ili tuwe na uzima tena tuwe nao tele.
Lakini kubwa zaidi alikuja ili kumkomboa mwanadamu katika dhambi.
Yesu anapokuwa moyoni mwako hiyo ndiyo chemchemi ya uzima ndani yako.
Unaposamehewa tu dhambi na moyo wako kuwa safi basi hata magonjwa yanakimbia.

ISAYA 33:24
Wala hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa; watu wakaao humo watasamehewa uovu wao.

****************
Hivyo Chemchemi za uzima zitakapokuwa moyoni mwako ambozo ni Yesu Kristo aliye msamaha wa dhambi basi kuugua kutakimbia kabisa, Yesu ndiye njia na kweli na UZIMA.
Uzima wa MTU upo ndani ya Yesu na ndiyo maana anasema pia aniaminiye mimi hata atakapokufa ataishi.
BWANA YESU ASIFIWE SANA.

ZABURI 119:11
Moyoni mwangu nimeliweka neno lako,Nisije nikakutenda dhambi.

****************
Huyu mwandishi wa Zaburi anasema ameliweka neno la Mungu moyoni ili asitende dhambi akiwa na maana kwamba ukishamweka Yesu (Neno) moyoni mwako hutatenda dhambi tena maana neno likijaa moyoni mwako kila utakachofanya biblia inakuwa ni muongozo mzuri sana kwako na utakapotii hutatenda dhambi.

Ukiwa na Yesu ndani yako atakupa Yule msaidizi ambaye ni Roho wa kweli aliyetuahidi na atatusaidia katika mambo yote.
Yesu ndiye aliyetuahidi sisi walio wake kwamba hatatuacha yatima bali atamwomba baba atupe msaidizi.
Sasa kama hujaokoka ili uwe wa Yesu naye akupe msaidizi wa kuishinda dhambi wala usijidanganye kwamba hutendi dhambi.

YEREMIA 17:9
Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?

*****************
Iko hivi
Kama hujaokoka basi hujampata Yesu katika maisha yako.
Na kama hujampata Yesu huna nguvu yoyote ya kushinda dhambi maana moyoni mwako neno halipo.
Na Yesu ndiye anayekupa Roho wa kukuongoza katika mambo yote.
Usijidanganye kwamba hutendi dhambi maana moyo ni mdanganyifu na kamwe wewe huwezi kuujuwa.
Wewe huna uwezo wowote wa kuujuwa moyo wako.
Yesu peke yake ndiye anayejuwa kama moyo wako ni mkamilifu au unakudanganya.
Yesu akiwa moyoni mwako ndipo utajijuwa kama una dhambi au huna.
Moyo unaweza kukuaminisha kitu cha ajabu sana wala usibadilishwe na mtu yeyote hivyo ili moyo wako uwe na kibali mbele za Mungu ni lazima ndani yake ulijaze neno lake, Yesu akae moyoni mwako kila wakati.

METHALI 18:12
Kabla ya uharibifu moyo wa mwanadamu hujivuna;Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu.

***************
Mtaji wa kwanza kwa mtu anayetaka kufanikiwa ni WAZO.
Lile wazo linatoka ndani ya moyo.
Sasa moyoni mwako Yesu yupo ili litoke wazo jema?
Kama shetani ndiye aliye moyoni mwako basi litatoka wazo baya tu.

Unapoona unatumia simu yako unaona ni jambo la kawaida ujue kuna mtu alianzisha wazo kutoka moyoni akalitendea Kazi.

Unapoona nchi yenye vita watu wanauwana ujue kuna mtu mmoja alitoa wazo moyoni mwake ambako hakukuwa na chemchemi za uzima ndiyo maana maovu yanatendeka.

Ukiona upo huru hutawaliwi ujue kuna mtu alitoa wazo moyoni mwake akaanza kupigania Uhuru watu wakakombolewa.

Unapomuona Yesu Kristo anatenda mambo kwetu makubwa na ya ajabu watu wanaokoka na kukombolewa katika maovu ujue ni Mungu aliwaza akaona amtoe mwanae wa pekee ili kila amwaminiye aokolewe katika yeye.

Ukiona mtu anateseka, anajuta, ameanguka, Hana amani, vita, na mambo mengine ya uharibifu basi ujue kabla ya mtu huyo kuwa hivyo moyo wake ulijivuna.
Shetani yuko hivi leo kwasababu alijiinua na kuwa na kiburi na majivuno moyoni mwake.

Ukiona mtu anaheshimika, amefanikiwa, ameokoka na kumpokea Yesu, amekuwa na utajiri udumuo na wenye amani, basi ujue moyo wake ulikuwa mnyenyekevu.

MATHAYO 11:29
Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

*****************
Yesu anasema tujifunze kwake, ni mpole na mnyenyekevu wa Moyo.
Raha tuliyo nayo na mamlaka tulizo nazo ni kutokana na unyenyekevu wa moyo wake.
Alitii yote hata mauti ya msalaba.
Hakuna mahali popote ambapo Yesu alikuwa mkaidi mpaka alipofika msalabani.
Ule unyenyekevu wa Moyo wake ndiyo uliomsaidia kushinda na dunia ikaokolewa.
BWANA YESU ASIFIWE SANA.

1WAFALME 11:1-3
Mfalme Sulemani akawapenda wanawake wengi wageni, pamoja na binti yake Farao, wanawake wa Wamoabi, na wa Waamoni, na wa Waedomi, na wa Wasidoni, na wa Wahiti,

na wa mataifa BWANA aliyowaambia wana wa Israeli, Msiingie kwao, wala wasiingie kwenu; kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao. Sulemani akaambatana nao kwa kuwapenda.

Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao wakeze wakamgeuza moyo.

*****************
Pamoja na Sulemani kumpenda Mungu lakini uharibifu ulipoingia moyoni mwake alibadilika mpaka kuabudu miungu.
Hakuulinda moyo wake.
Unapokuwa na mahusiano na mwanamke huwa mnakuwa mwili mmoja hivyo unakuwa na tabia za kwake na utajikuta unafanana naye.
Linda moyo wako kuliko yote ulindayo.
Dhambi zote zinaanzia moyoni.

LUKA 6:45
Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.

*****************
Ukitaka kumjuwa mtu ana tabia gani moyoni mwake au anawaza nini basi msikilize maneno yake.
Moyo husema kupitia kinywa maana ulimi hufichua siri za moyoni.
Ukiwa na kitu moyoni halafu ukakaa na mtu mkaongea kwa dakika chache atajuwa kilichopo moyoni mwako.
Kama una kisasi na mimi ukikaa na mimi tukiongea lazima nitakujuwa tu.
Kama unanipenda nikikaa nikiongea na wewe nitakujuwa tu.
Kama nikisikiliza wingi wa maneno yako ukawa unaongelea jambo fulani tu basi dhahiri hayo ndiyo maisha yako.

MATHAYO 9:20-22
Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake.

Kwa maana alisema moyoni mwake, Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona.

Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu; imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile.

******************

Tazama wazo la moyoni la huyu mwanamke namna lilivyobadili kabisa historia ya maisha yake.
Mawazo ya moyo wa huyu mwanamke yalikuwa ni uponyaji kupitia Yesu Kristo na alimweka moyoni akamwamini na kweli akapata uponyaji na Yesu akawa ndani yake.

Sasa wewe umemweka nani moyoni mwako juu ya changamoto ulizo nazo?
JIPANGE.
Kilichopo moyoni mwako ndicho kitakachokukomboa.

MATHAYO 6:21
kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako.

******************
Kwa sasa unamtumikia nani?
Unamwamini nani katika maisha yako?
Umeweka hazina yako kwa waganga?
Umejiwekea hazina yako kwa wanadamu?
Kila unachofanya utalipwa haijalishi ni kibaya au kizuri.
Kama ukifanya mema Mungu Baba kwa jina la Yesu Kristo atakulipa mema.
Lakini ukifanya uovu utalipwa na huyo huyo mwovu.
Weka hazina yako kwa Yesu Kristo nawe utaikuta Mbinguni mpendwa.
Maisha haya ni mafupi sana hayakawii kwisha.
Ulikojiwekea hazina yako ndiko moyo wako uliko.
LINDA SANA MOYO WAKO.

KUSHINDA DHAMBI

ZABURI 19:14
Maneno ya kinywa changu,Na mawazo ya moyo wangu,Yapate kibali mbele zako, Ee BWANA,Mwamba wangu, na mwokozi wangu.

****************
Tumeshaona chanzo cha jambo lolote kuwa ni mawazo ya moyo.
Hata shetani anapotaka kukuingia huwa anakupa wazo halafu unapoanza kulitafakari anakupa majibu na kisha unatenda.

Mfano mzuri ni mawazo ya kuzini huwa ni mabaya sana.
Unaweza ukawa umekaa unaanza kuwaza ngono tu moyoni mwako.
Sasa ukiendelea kuwaza kwa muda Fulani na mwili unapokea lile ombi kisha unajikuta umeshazama kabisa na kutoka hutaweza tena.

WAEFESO 4:27
wala msimpe Ibilisi nafasi.

***************
Unapojipa nafasi ya kuwaza uovu kwa muda mchache huwa shetani anakupa mbinu za ushindi na utajikuta tu umechukua maamuzi.

Ukijiona tu kuna wazo linaingia moyoni mwako ambalo halina kibali mbele za Mungu au halimpendezi Mungu basi usijipe kabisa hata sekunde kumi za kuendelea kulichanganyua.
Kama ukiendelea kulitafakari utafanya maamuzi yasiyo na kibali mbele za Mungu na utakuja kujuta baadae.
Kabla hujaongea chochote kwanza jiulize Mungu atafurahia nachokisema?
Mwandishi ameanza kumwomba Mungu kuhusu maneno ya kinywa chake maana ukishaanza kuongea uovu ndipo na moyo utatafakari huo uovu na shetani huja kuutia nguvu ili ufanye maamuzi yasiyo mpendeza Mungu.
Kama huamini anza sasa kuwaza jambo fulani kwa muda wa dakika kumi bila kuingiza mawazo mengine yoyote uone utachukua maamuzi gani.
Halafu kama kuna tabia Fulani imekushinda kabisa kuiacha anza leo, ukiona wazo la kufanya ile tabia linakujia usilifikirie tena uone kama utaifanya tena.

Hata watu wa matangazo huwa wanatumia mbinu hii.
Wanarusha tangazo lao kwenye vyombo vyote vya habari.
Halafu linakuwa linarushwa kila wakati na watu wanashawishika na kujikuta hata wamekaririshwa kwa lazima na ukishaanza kuliwazia kwa undani utanunua ile bidhaa au utaona ni bora japo hutaki au huna fedha za kununulia.
Kama usingeendelea kusikiliza yale matangazo wala usingeipenda ile bidhaa.

Kuna wimbo ulipousikia kwa mara ya kwanza uliuona sio mzuri masikioni mwako lakini baada ya kuusikia mara kwa mara mpaka umejikuta sasa hivi umeufanya mwito wa simu yako.
Kama usingekuwa unaendelea kuusikia bila Shaka usingeupenda.

Jizuie kuwaza uovu pindi tu wazo la huo uovu linapokujia na utafanikiwa kuishinda dhambi.
BWANA YESU ASIFIWE SANA.

#Powered_By_Holly_Spirit

No comments:

Post a Comment