Thursday, 10 May 2018

MUNGU HUBARIKI KULINGANA NA MAPENZI YAKE NA NJIA ZAKE SI NJIA ZETU. PIA AKILI ZAKE HAZICHUNGUZIKI.

BWANA YESU ASIFIWE SANA.

Leo nakuletea somo lenye kichwa kinachosema,

MUNGU HUBARIKI KULINGANA NA MAPENZI YAKE NA NJIA ZAKE SI NJIA ZETU.
PIA AKILI ZAKE HAZICHUNGUZIKI.

Lengo la Mungu kumuumba mwanadamu pamoja na vyote alivyopendezwa navyo kwamba viwepo ni ili vimwabudu tu.
Hukuumbwa kwaajili ya kufanya jambo lingine lolote pasipo kulitukuza jina lake.

WAKOLOSAI 3:17
Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.

**** **** ****
Haijalishi unafanya mizaha,
Haijalishi unaongea na marafiki zako,
Haijalishi unajenga nyumba,
Wala haijalishi unafanya jambo gani.
Lazima ufanye kwa jina la Bwana Yesu.

Vyote mwanadamu anavyovihangaikia hapa duniani vinatakiwa viwe ni matokeo ya kumwabudu Mungu na siyo umwabudu ili akupe hivyo vitu.
Unaweza ukamtafuta sana Mungu kwa muda mrefu ukahisi bado hujabarikiwa lakini nakuambia Mungu anabariki jinsi apendavyo.
Unaweza ukawa umeshabarikiwa lakini kulingana na namna unavyojiona na watu wanavyokuona unahisi bado hujabarikiwa.
Unachotakiwa kushikilia kwenye akili yako ni kwamba,

Mungu akupe mali au la asikupe mali ni lazima umwabudu yeye.

Akupe hitaji lako, la asikupe ni lazima umwabudu yeye tu.

Akubariki la asikubariki ni lazima umwabudu yeye.

Mtume PAULO alikuwa na nguvu nyingi sana za Mungu ndani yake.
Lakini pamoja na hayo pia alikuwa na udhaifu ndani ya mwili wake.
Uthaifu aliokuwa nao PAULO ni udhaifu ambao aliweza kuuondoa katika mwili wa mtu mwingine kwa jina la YESU na huyo mtu akapokea uponyaji akapona.
Lakini kwake ilishindikana kuuondoa kwa jina la huyo huyo YESU.

2WAKORINTHO 12:7-10
Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi.

 Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke.

 Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.

 Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.

**** **** ****

Mungu akawa anajisifu na udhaifu wa PAULO kwamba uweza wake utatimilika ndani ya udhaifu huo huo.

Je, Paulo alikuwa hajabarikiwa na Mungu?

Unaweza ukawa karibu sana na Mungu lakini bado ukawa na mizigo ya changamoto usizoweza kuziepuka katika maisha yako.
Shetani atakubeza (Mungu wako yuko wapi katika hili unalopitia?)
Ili usijisifu tena na huyo Mungu.
Lakini mwambie shetani kwa ujasiri kwamba "MUNGU HUBARIKI KWA MAPENZI YAKE"
Hata sasa Mungu yupo na mimi na ninatembea katika baraka zake.
Na jinsi mwanadamu aonavyo sivyo Mungu aonavyo.
Ilimradi unaishi katika kusudi la Mungu kukuumba wewe la kumtumikia na kumwabudu yeye peke yake.
Ikiwa unaishi kwa misingi ya neno lake basi usijali changamoto na kejeli zozote za shetani wewe amini Mungu yuko na wewe na amekushika mkono.

TWENDE SASA KWENYE NENO LA MSINGI WA MAFUNDISHO YETU.

ISAYA 55:8
Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema BWANA.

**** **** ****
Hilo ndilo neno letu la msingi wa MAFUNDISHO yetu. Tuangalie Roho Mtakatifu anatufundisha nini juu ya hili neno.

Unapomwabudu Mungu kwaajili ya shida fulani unakuwa kama unamtaka MUNGU ainunue haki yake kutoka kwako.
Utakuwa kama unataka kumhonga kitu ambacho ni haki yake.
MUNGU ni MUNGU tu na anapaswa kuabudiwa hata kama hajatatua changamoto zako isikiondoe wewe katika kusudi la yeye kukuumba.
Hata kama humtimizii mtoto wako mahitaji yake yote haitaubadilisha ukweli uliopo kwamba wewe ni baba yake.
Atakuamkia shikamoo baba,
Atakuheshimu na hataweza kubadili damu usiwe baba yake.

MUNGU HUBARIKI KWA MAPENZI YAKE JINSI APENDAVYO YEYE.
lakini zote ni baraka.

Mwenye maono amebarikiwa
Anaeponya kwa jina la YESU amebarikiwa
Mwenye Mali amebarikiwa na mwenye afya nzuri pia amebarikiwa.
Yupo mwenye treni, meli, ndege na migodi ya madini ambae amebarikiwa na Mungu ikiwa analiishi neno lake.
Lakini yupo pia mwenye mifugo, mashamba, familia imara na Hana elimu naye amebarikiwa.
Wote wamebarikiwa KULINGANA na MAPENZI ya MUNGU.

MATHAYO 4:10
Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.

**** **** ****
Tunachokiangalia tu ili tujue tumebarikiwa ama hatujabarikiwa ni je,
Tunaishi katika misingi ya NENO la MUNGU?
Kama unapitia changamoto na vikwazo vingi na wakati huo unamwabudu Mungu wala usitishike na hizo changamoto.
Hata Yesu huyo mjaribu alimjia kwakuwa alikuwa kwenye wakati mgumu lakini yeye hakutoka katika kusudi la Mungu.
Alimshinda kwa NENO.

JIFUNZE SASA NAMNA AMBAVYO MAWAZO YA MUNGU YALIVYO TOFAUTI NA MAWAZO YETU.

YOSHUA 24:2-3
Yoshua akawaambia watu wote, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Baba zenu hapo zamani walikaa ng’ambo ya Mto, maana Tera, baba yake Ibrahimu, naye ni baba yake Nahori; wakaitumikia miungu mingine.

 Nami nikamtwaa Ibrahimu baba yenu toka ng’ambo ya Mto, nikamwongoza katika nchi yote ya Kanaani; nikaongeza uzao wake, nikampa Isaka.

**** **** ****
Mungu alimtoa Ibrahimu ndani ya nyumba ya baba yake Tera waliokuwa wanaabudu miungu.
Lengo la Mungu ni kumtengeneza Ibrahimu  aanzishe uzao mwingine ambao ungemtumikia na kumwabudu yeye.

Asilimia kubwa watu waliabudu miungu mingine na hilo jambo halikumpendeza Mungu aliye hai.

MWANZO 12:1-3
BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha;

 nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka;

 nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.

**** **** ****
Hizi ni baraka za ajabu sana ambazo alikuwa anazijuwa Abram peke yake pamoja na Mungu aliyemwahidi.
Na alikuwa anajijuwa kwamba amebarikiwa kwa kiwango kikubwa sana.
Lakini hakujuwa kuwa hizo baraka zitakuwa za aina gani.
Akayafuata maagizo ya Mungu akajitenga na nyumba ya baba yake Tiro waliokuwa waabudu miungu.
Akaenda kumwabudu Mungu aliye hai.

MWANZO 13:15-16
maana nchi hii yote uionayo, nitakupa wewe na uzao wako hata milele.

 Na uzao wako nitaufanya uwe kama mavumbi ya nchi; hata mtu akiweza kuyahesabu mavumbi ya nchi, uzao wako nao utahesabika.

**** **** ****
Mungu anamthibitishia Ibrahimu kwamba uzao wake utakuwa kama muvumbi yasiyohesabika.
Amembariki kuwa na uzao mkubwa sana. Ni agano la Mungu na Ibrahimu peke yake. Lakini cha kushangaza mkewe Ibrahimu akawa hapati mimba.
Ikawa changamoto kwake japo anaziishi baraka za Bwana maishani mwake.

Ibrahimu alifika hatua ya kuzaa na kijakazi wake baada ya kuona kama Sara hawezi tena kuzaa, ameshakuwa mzee.
Lakini hayo yalikuwa ni macho yake na sivyo kama aonavyo Mungu.

MWANZO 17:17
Ndipo Ibrahimu akaanguka kifudifudi akacheka, akasema moyoni, Je! Mtu wa umri wa miaka mia, kwake atazaliwa mtoto? Naye Sara mwenye umri wa miaka tisini atazaa?

**** **** ****
Wanadamu wanaweza kuona kama hujabarikiwa lakini umebarikiwa.

Unaweza ukajiona hujabarikiwa lakini umebarikiwa.

Changamoto na vitisho vya maneno ya watu visikutoe katika mpango wa Mungu.
Vyovyote utakavyokuwa unaendelea kumwamini Mungu hata kama unachekwa na watu.
Baraka zako zipo na umeshabarikiwa.
Endelea na hilo tumaini lako la milele.

MWANZO 18:12-14
Kwa hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu mzee?

 BWANA akamwambia Ibrahimu, Mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee?

 Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda BWANA? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani.

*** **** ****
Haijalishi unajionaje.
Haijalishi wanadamu wanakuonaje.
Bali inajalisha unaishi kwa misingi gani ndiyo ushindi wako.
Ikiwa tumaini lako ni kwa Mungu aliye juu basi hutapungukiwa kwake.
Wanadamu wanaweza kukuona umepungukiwa au dhaifu lakini kwa Mungu wewe ni hodari.

Njia zake hazichunguziki wala hawazi kile unachowazia wewe.
Ikiwa unamtumainia yeye amini umebarikiwa wala usitafute kutazamwa na wanadamu ikiwa yeye ameshakutazama na mkono wake umekushika.

MWANZO 21:1-3
BWANA akamjia Sara kama alivyonena, na BWANA akamfanyia kama alivyosema.

  Sara akapata mimba akamzalia Ibrahimu mwana wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu.

 Ibrahimu akamwita jina lake Isaka, yule mwana aliyezaliwa, ambaye Sara alimzalia.

**** **** ****
Kwa mazingira ya kawaida watu waliosikia kwa Ibrahimu kwamba amebarikiwa na atakuwa taifa kubwa lazima waliugua kwa kicheko.
Walicheka sana kuona amezaa mtoto uzeeni tena mmoja.

MWANZO 22:15-18
Malaika wa BWANA akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni

 akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee,

 katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao;

 na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.

**** **** ****
Mungu anaapa na nafsi yake tena anamwapia mwanadamu na kumwambia atambariki.
Atambariki kwakuwa ametii maneno na sauti yake.
Amemfuata kumtumikia yeye.
Kama Mungu anaapa kuna nini tena?
Halafu angalia hapa anamwambia atambariki kwa kitu gani.
Atambariki katika uzao.
Kama nyota za mbinguni au mchanga ulioko pwani.
Yani atakuwa taifa kubwa.
Hapo Ibrahimu ameshabarikiwa kwa kuwa ameisikia sauti ya Mungu.

Cha kushangaza Sara alifariki na Ibrahimu akafariki bila kuziona hizo baraka. Wote Ibrahimu na Sara walifariki wakiwa na huyo mtoto mmoja tu wa ahadi ambaye ni Isaka.

Unafikiri wanadamu waliongea maneno mangapi?
Unadhani walikejeli kwa kiasi gani baraka alizosema amebarikiwa na Mungu?

Je Ibrahimu alikuwa amebarikiwa au hakubarikiwa?
Unahisi umebarikiwa au hujabarikiwa?

MWANZO 21:10-12
Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka.

 Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe.

 Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa.

**** **** ****
Kumbe unapobarikiwa wewe hata uzao wako utabarikiwa.
Humbe baraka huwa zinarithiwa.
Katika baraka zote Mungu alizomwahidi Ibrahimu hakuziona kabisa mpaka kufa kwake

 (Lakini alikuwa amebarikiwa)

Hapa Mungu anakuja kumwambia tena Ibrahimu kwamba Isaka amezirithi baraka zile.
Ule uzao alioahidiwa ataurithi Isaka.

TUANGALIE MUNGU ANASEMAJE KUHUSU ISAKA BAADA YA IBRAHIMU KUFARIKI.

MWANZO 25:11
Ikawa, baada ya kufa kwake Ibrahimu, Mungu akambariki Isaka mwanawe. Naye Isaka akakaa karibu ya Beer-lahai-roi.Uzao wa Ishmaeli.

**** **** ****
Hapa ndipo napojua kuwa akili za Mungu hazichunguziki kabisa.

Tuendelee kuangalia maajabu ya Mungu.

MWANZO 26:3-5
Kaa ugenini katika nchi hiyo, nami nitakuwa pamoja nawe, na kukubariki, maana nitakupa wewe na uzao wako nchi hizi zote. Nami nitakifanya imara kiapo nilichomwapia Ibrahimu baba yako.

 Nitazidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, nami nitawapa uzao wako nchi hizi zote, na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia.

 Kwa sababu Ibrahimu alisikia sauti yangu, akayahifadhi maagizo yangu, na amri zangu, na hukumu zangu, na sheria zangu.

**** **** ****

Mungu anamwahidi tena Isaka ahadi ile ile aliyomwahidi Ibrahimu baba yake.

MWANZO 26:24
BWANA akamtokea usiku ule ule, akasema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu baba yako, usiogope, maana mimi ni pamoja nawe, nami nitakubarikia, na kuzidisha uzao wako kwaajili ya Ibrahimu mtumishi wangu.

**** **** ****

Kumtumikia kwako Mungu Leo kunaweza kuwa ni kama hazina na urithi kwa wanao.
Au uzee wako.
Maombi unayoomba Leo kwa kufunga yanaweza yakakusaidia baadae katika uzee wako wakati ambao huna tena uwezo wa kufunga kwaajili ya udhaifu wa mwili wako.
Unaweza ukaomba Mungu akubariki Leo ukawa unazishika hukumu zake lakini hizo baraka zikaja kuangukia kwa watoto wako.

MWANZO 25:21-27
Isaka akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye BWANA akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba.

 Watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda kumwuliza BWANA.

 BWANA akamwambia,Mataifa mawili yako tumboni mwako,Na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni mwako.Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili,Na mkubwa atamtumikia mdogo.

Siku zake za kuzaa zilipotimia, tazama! Mapacha walikuwamo tumboni mwake.

 Wa kwanza akatoka, naye alikuwa mwekundu mwili wote kama vazi la nywele. Wakamwita jina lake Esau.

 Baadaye ndugu yake akatoka, na mkono wake unamshika Esau kisigino. Akaitwa jina lake Yakobo. Isaka alikuwa mwenye miaka sitini mkewe alipowazaa.

 Watoto wakakua, Esau alikuwa mtu ajuaye kuwinda wanyama, mtu wa nyikani, na Yakobo alikuwa mtu mtulivu, mwenye kukaa hemani.

**** **** ****
Baada ya hawa watoto kuzaliwa Isaka alimbariki Yakobo.
Yakobo akashikilia urithi naye Isaka akafa kabla hajaliona hilo taifa kubwa lenye watu wasiyohesabika.

Akabaki Yakobo akitembelea kile kijiti cha zile baraka za Ibrahimu babu yake.

MWANZO 28:10-14
Yakobo akatoka Beer-sheba, kwenda Harani.

 Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale.

 Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake.

 Na tazama, BWANA amesimama juu yake, akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako.

Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa.

**** **** ****
Yani mtu wa Mungu kama hujalisoma neno na kujifunza kwa bidii unaweza ukajihisi unalala na njaa kumbe umeshakula na umeshiba mno.
Unaweza ukamlalamikia Mungu kumbe ameshakupa mahitaji yako yote.
Usichoke kuomba wala usimpangie Mungu namna ya kuachia baraka zake katika maisha yako.
Mimi nimebarikiwa maana tumaini langu ni kwake yeye.
Omba Leo huenda wakafaidika watoto wako, wazazi wako, wajukuu hata vitukuu.

Lakini ikiwa ni kwa MAPENZI ya Mungu hata wewe unaweza kuyaishi maombi yako ya Leo.
Tulia na Mungu mwache atimize MAPENZI yake usimpangie.
Lakini pia yeye hubadili majira na nyakati.
Huzuru wafalme na nuru hukaa kwake.

Ahadi za Ibrahimu hakuzishuhudia na macho yake,
Ibrahimu akamuachia Isaka naye hakuzishuhudia kwa macho yake,
Isaka akamwachia Yakobo.

Hapa MUNGU anamtamkia Yakobo baraka zile zile alizomtamkia Ibrahimu.

Ni miaka mingi sana imeshapita lakini bado wanaishi kwenye kusudi la Mungu bila kujali kitatokea lini.

Tuone itakuwaje.

Halafu hizi roho za kufuatilia huwa zipo kabisa.

Tazama Ibrahimu alipata mtoto kwa shida sana yeye na Sara.

Isaka naye mke wake Rebeka alikuwa tasa na walipata uzao baada ya Isaka kumwomba BWANA juu ya mke wake.

Yakobo naye alikaa muda mrefu na Raheli bila kupata mtoto,
Baada ya kumwomba sana Mungu ndipo akamzaa Yusufu.

Raheli alijaribu pia kufanya kama Sara akamwambia Yakobo ampe uzao kwa mjakazi wake aliyeitwa Bilha.

Wote wawili Bilha na Lea aliyekuwa mdogo wake Raheli walizaa watoto wengi lakini utithi wa zile baraka za Mungu kwa Ibrahimu zilienda kwa Yusufu aliyekuwa mtoto wa Raheli.

Yakobo alikuwa na wanawake wawili ambapo mmoja ndiye aliyekuwa wa malengo yake aliyeitwa Raheli.
Huyo Lea alikuwa mke wake pia kwaajili ya Labani ambaye ni mjomba wake Yakobo kufanya hila na kumwozesha watoto wake wote wawili.

SOMA MWANZO SURA 28 MPAKA 30 YOTE.

MWANZO 35:9-12
Mungu akamtokea Yakobo tena, aliporudi kutoka Padan-aramu akambariki.

 Mungu akamwambia, Jina lako ni Yakobo; hutaitwa tena Yakobo, lakini Israeli litakuwa jina lako. Akamwita jina lake, Israeli.

 Mungu akamwambia, Mimi ni Mungu , uzidi ukaongezeke. Taifa na kundi la mataifa watatoka kwako, na wafalme watatoka viunoni mwako.

 Na nchi hii niliyowapa Ibrahimu na Isaka nitakupa wewe, na uzao wako baada yako nitawapa nchi hiyo.

**** **** ****
Hakuna tofauti yoyote katika hizi ahadi za kubarikiwa.
Lakini hakuna aliyezishughudia hizi baraka kwa macho yake.
Kati ya Ibrahimu, Isaka, na Yakobo.

Lakini wanamtumikia na kumwabudu Mungu kwa uaminifu.

TUENDELEE

Yakobo alizaa watoto 12 ambaye haitwi tena Yakobo Mungu alishambadilisha jina na kumwita Israeli

 MWANZO 35:10

Kwahiyo sasa Yakobo tutamwita Israeli.

Ule urithi wa zile baraka za Ibrahimu ukaenda kwa  Yusufu mtoto wake Israel.

Kwahiyo Yusufu akawa ndiye anatembelea zile baraka na ahadi ya Mungu.

Yusufu yupo katika ahadi na baraka zote za Mungu lakini angalia kilichompata katika maisha yake.

Utahisi labda hajabarikiwa.

Ndugu zake walipogundua kuwa amebarikiwa na Mungu wakaamua kumwuza Misri kwa kuwa mtumwa ili ndoto yake isitimie.

MWANZO 37:5-8
Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia;

 akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota.

 Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu.

 Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake.

**** **** ****

Ndugu zake walijisikia vibaya juu ya ile ndoto yake wakapanga kumwuza kuwa mtumwa huko Misri.

MWANZO 37:26-28
Yuda akawaambia ndugu zake, Kwafaa nini kumwua ndugu yetu, na kuificha damu yake?

 Haya, na tumwuze kwa hawa Waishmaeli, wala mikono yetu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu, na damu yetu. Ndugu zake wakakubali.

 Wakapita wafanya biashara Wamidiani; basi wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika birika, wakamwuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri.

**** **** ****

Ndugu zake walifanikiwa kumwuza na kuwa mtumwa kule Misri.

Lakini kwakuwa alikuwa na ahadi ya Mungu katika maisha yake alipata kibali machoni pa Farao.

Baadae njaa ikatokea dunia nzima ila Misri.

Njaa iliyowafanya ndugu wa Yusufu kwenda Misri kujitafutia chakula kwa kununua.

MWANZO 42:3-4
Basi ndugu kumi wa Yusufu wakashuka Misri ili wanunue nafaka.

 Walakini Benyamini, ndugu wa Yusufu, Yakobo hakumpeleka pamoja na ndugu zake, maana alisema, Mabaya yasimpate.

**** **** ****
Ndugu wa Yusufu walioshuka Misri walikuwa 10 akabaki Benyamini.
Kwahiyo ukijumlisha na Yusufu wanakuwa 12 ambao wote ni wana wa Yakobo(Israeli)

MWANZO 42:6-9
Naye Yusufu alikuwa ni liwali juu ya nchi, ndiye aliyewauzia watu wote wa nchi. Nao ndugu zake Yusufu wakaja, wakainama kifudifudi mbele yake.

 Yusufu akawaona nduguze, akawatambua, lakini alijifanya kama mgeni kwao. Akasema nao kwa maneno makali, akawaambia, Mmetoka wapi ninyi? Wakasema. Tumetoka nchi ya Kanaani, ili tununue chakula.

 Yusufu akawatambua nduguze, bali wao hawakumtambua yeye.

 Yusufu akazikumbuka zile ndoto alizowaotea. Akawaambia, Wapelelezi ninyi, mmekuja ili mwuone utupu wa nchi.

**** **** ****
Baada ya Yusufu kufungwa gerezani miaka mingi lakini baadae Mungu akampa kibali akamketisha na wakuu na hatimaye akawa liwali juuu ya Misri yote.
Tena alifungwa kwa kesi ya kusingiziwa.

Je, ni nani awezaye kupatwa na changamoto zote hizo halafu akajiona au watu wakamwona mbarikiwa?

Je, hawataanza kukukejeli wewe na Mungu unayemtumikia?

Ukijiona umesimama vizuri na Mungu usiangalie unachopitia wewe amini Mungu amekushika mkono.

TUENDELEE KUANGALIA ZILE BARAKA ZA IBRAHIMU ZIKO WAPI.

MWANZO 45:17-20
Farao akamwambia Yusufu, Uwaambie ndugu zako, Fanyeni hivi; wachukuzeni mizigo wanyama wenu, mwondoke mwende nchi ya Kanaani;

 kisha mkamtwae baba yenu, na watu wa nyumbani mwenu, mkanijie; nami nitawapa mema ya nchi ya Misri, nanyi mtakula unono wa nchi.

 Nawe umeamriwa; fanyeni hivi, mjitwalie magari katika nchi ya Misri kwa watoto wenu wadogo na wake zenu, mkamchukue baba yenu mje.

 Wala msivisumbukie vyombo vyenu, maana mema ya nchi yote ya Misri ni yenu.

**** **** ****
MWANZO 46:1-4
Akasafiri Israeli, pamoja na yote aliyokuwa nayo, akaja Beer-sheba, akamchinjia sadaka Mungu wa Isaka babaye.

 Mungu akanena na Israeli katika ndoto ya usiku, akasema, Yakobo, Yakobo. Akasema, Mimi hapa.

 Akasema, Mimi ni Mungu, Mungu wa baba yako, usiogope kushuka mpaka Misri; maana nitakufanya uwe taifa kubwa huko.

 Mimi nitashuka pamoja nawe mpaka Misri; nami nitakupandisha tena bila shaka; na Yusufu ataweka mkono wake juu ya macho yako.

**** **** ****
Hapa sasa uzao mzima wa Ibrahimu wanashuka Misri na bado Mungu anamwahidi Israeli kwamba atamfanya kuwa taifa kubwa huko Misri.

MWANZO 47:5-6
Farao akamwambia Yusufu, akisema, Baba yako na ndugu zako wamekujia;

 nchi ya Misri iko mbele yako, palipo pema pa nchi uwakalishe baba yako na ndugu zako; na wakae katika nchi ya Gosheni. Tena ukijua ya kuwa wako watu hodari miongoni mwao, uwaweke wawe wakuu wa wanyama wangu.

**** **** ****
Israeli na wanawe wote 12 wakawa wanaishi Misri kwa kuikimbia njaa nchi ya Kanaani.
Na Mungu alishamwahidi kwenye ndoto kwamba atamfanya huko kuwa taifa kubwa.

MWANZO 48:21
Israeli akamwambia Yusufu, Angalia, mimi ninakufa, lakini Mungu atakuwa pamoja nanyi, naye atawarudisha mpaka nchi ya baba zenu.

**** **** ****
Nchi ya baba yao Ibrahimu na Isaka ni nchi ya Kanaani na Israel anamwambia Yusufu kwamba Mungu atakuwa pamoja nao na watarudi.

Israeli akafa na Yusufu naye akafa, uzao wa wana wa Israeli ukaongezeka huko Misri

KUTOKA 1:6-9
Yusufu akafa, na ndugu zake wote, na watu wote wa kizazi kile.

 Na wana wa Israeli walikuwa na uzazi sana, na kuongezeka mno, na kuzidi kuwa wengi, nao wakaendelea na kuongezeka nguvu; na ile nchi ilikuwa imejawa na wao.Waisraeli Wateswa

 Basi akainuka mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu.

 Akawaambia watu wake, Angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi tena wana nguvu kuliko sisi.

**** **** ****
Ule uzao uliongezeka isivyo kawaida mpaka wamisri wakawa na hofu kwamba watakuja kutawaliwa.

Wamisri wakawanyanyasa sana na kuwapa kazi ngumu.
Wakawa watumwa.

Walilia usiku na mchana kwa yale mateso waliyoyapata.
Pamoja na changamoto zote za kuteseka na kutumikishwa kazi ngumu lakini bado walikuwa na ahadi ya Mungu katika maisha yao.
Ni watu waliobarikiwa.
Pamoja na kubarikiwa kwao lakini walikuwa ni watu waliodharauliwa sana.

KUTOKA 1:15-17
Kisha mfalme wa Misri akasema na wazalisha wa Waebrania, mmoja jina lake aliitwa Shifra, na wa pili jina lake aliitwa Pua;

 akasema, Wakati mwazalishapo wanawake wa Kiebrania na kuwaona wa katika kuzaa, ikiwa ni mtoto mwanamume, basi mwueni, bali ikiwa ni mtoto mwanamke, na aishi.

 Lakini wale wazalisha walikuwa wakimcha Mungu, wasifanye kama walivyoamriwa na huyo mfalme wa Misri, lakini wakawahifadhi hai wale wanaume.

**** **** ****
Wamisri walitafuta kila njia za kuwapunguza ikashindikana.
Ahadi ya Mungu kwa Ibrahimu inaanza kuonekana.
Zile baraka za kuwa taifa kubwa ndiyo zinaanza kuonekana sasa.

(Mungu hubariki kwa mapenzi yake na njia zake hazichunguziki)

KUTOKA 2:5-10
Basi binti Farao akashuka, aoge mtoni, na vijakazi wake wakatembea kando ya mto; naye akakiona kile kisafina katika majani, akamtuma kijakazi wake kwenda kukileta.

 Akakifungua, akamwona mtoto, na tazama, mtoto yule analia. Basi akamhurumia, akasema, Huyu ni mmojawapo wa watoto wa Waebrania.

Basi umbu lake mtoto akamwambia binti Farao, Je! Niende nikamwite mlezi katika wanawake wa Kiebrania, aje kwako, akunyonyeshee mtoto huyu?

Binti Farao akamwambia, Haya! Enenda. Yule kijana akaenda akamwita mama yake yule mtoto.

Binti Farao akamwambia, Mchukue mtoto huyu, ukaninyonyeshee, nami nitakupa mshahara wako. Yule mwanamke akamtwaa mtoto, akamnyonyesha.

Mtoto akakua, naye akamleta kwa binti Farao, akawa mwanawe. Akamwita jina lake Musa, akasema, Ni kwa sababu nalimtoa majini.

**** **** ****
Katika Mungu kuitimiza ahadi yake kwa Ibrahimu akamwinua Musa naye akamtuma kwenda kuwatoa wana wa israeli kutoka huko utumwani Misri walikokuwa wanateseka.

Wakavuka bahari kwa ishara na ajabu nyingi.

Mpaka Leo hii sisi tulio wakristo ndiyo uzao wa Ibrahimu.

Je, sisi ni taifa kubwa au siyo?

Baraka alizoahidiwa Ibrahimu ndizo zilikuja kutimia kwa (YAKOBO)Israeli.

Ndiye huyo Mungu tunayemwabudu sisi Mungu wa Israeli.

Unaweza ukahisi hujabarikiwa kulingana na maisha unayoishi.

Ibrahimu aliamini kubarikiwa na kuwa taifa kubwa japo alikuwa na mtoto mmoja tu wa ahadi na akafa bila kuona chochote.

Ikiwa wewe unamwabudu Mungu kwa kweli na uaminifu amini hauko peke yako.

Ilimradi uwe mwaminifu mbele zake.
Kama ungefunuliwa macho yako Mungu akuonyeshe baraka zilizopo mbele yako ungemtukuza Mungu mchana na usiku.
Hata kama umekuwa mwaminifu kwa Mungu kwa muda mrefu na hujaona chochote mpaka uzeeni, wewe amini baraka zako zipo na usimpangie Mungu namna au majira ya kuzidhihirisha au kuzithibitisha hizo baraka.

ENDELEA KUMWABUDU MUNGU MAANA WEWE NI MBARIKIWA KWA JINA LA YESU KRISTO.

MUNGU HAMTUPI MTU.
BALI HUBARIKI KWA MAPENZI YAKE NA WAKATI WAKE.
NA PIA ANASEMA NJIA ZAKE SI KAMA ZETU NA AKILI ZAKE HAZICHUNGUZIKI.

#Powered_by_Holly_Spirt

1 comment:

  1. Amen ninejifunza na kuongezeka imani ya kukaza kumwabudu Mungu

    ReplyDelete