Monday, 4 June 2018

NGUVU NA THAMANI YA MWANADAMU (MTEULE)

NAKUSALIMU KWA JINA LA YESU KRISTO

Ni matumaini yangu ya kuwa u mzima wa afya ya Roho na akili mpaka muda huu ambao tumepata tena kibali mbele za Mungu kwa msaada wa Roho mtakatifu tukajifunze tena habari njema kabisa za ufalme wa mbinguni.

Leo tunajifunza somo lenye kichwa kinachoitwa,

NGUVU NA THAMANI YA MWANADAMU
                        (MTEULE)

Napozungumzia nguvu ya mwanadamu halafu kwenye mabano (MTEULE), Namaanisha kwamba watu wote waliopo duniani ni watu wa Mungu lakini MTEULE ni tofauti maana yeye siyo mtu wa Mungu tu bali ni mtoto wa Mungu.

YOHANA 1:12
Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;

************
Inamaana kama hujampokea Yesu bado hujapata huo uwezo wa kufanyika mtoto wa Mungu na wala wewe siyo MTEULE.

Unapokuwa umeokoka ndipo unaweza kusimama kwa ujasiri na kulitaja jina la Yesu na ndipo utakuwa na mamlaka ya kutumia mamlaka iliyopo ndani ya hilo jina.
Ukishapewa uwezo wa kufanyika kuwa mtoto wa Mungu ndipo utakuwa na kibali cha kutumia vitu vya Mungu ambaye kwa wakati huo atakuwa ni Baba yako.

Utakubaliana na mimi kwamba mtoto wa jirani yako hawezi kuja kwako na kuanza kutumia vitu vyako maana wewe siyo baba yake, lakini vitu vya baba yake ana uwezo wa kuvitumia na siyo kutumia tu bali pia ni urithi wake.
BWANA YESU ASIFIWE SANA.

Usije ukawa hujaokoka halafu ukaukuta mstari katika biblia halafu ukaanza kuutumia huku ukijifariji kwamba hata wewe unaweza kuutumia na ukawa tumaini lako.
Hizo mamlaka na nguvu na uweza uliopo katika hilo neno ni kwa watoto wake tu yeye aliye Baba yao.

Kama huelewi nachomaanisha tazama hapa.

MATENDO YA MITUME 19:13-16
Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo.

Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo.

Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani?

Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa.

*********************

Hawa walilitumia jina la Yesu wakidhani kila MTU anaweza akalitumia.
Walikuwa hawajaokoka.
Sasa usije ukajifariji kujipa imani kwa kumtaja taja Yesu katika matatizo yako halafu hujaokoka wala hujafanyika kuwa mtoto wake ukadhani itakusaidia kitu.
Walio wake anawajuwa.
BWANA YESU ASIFIWE SANA.

Hapo nilikuwa najitahidi tu kukupa utangulizi ili ujue maana ya (MTEULE)  ni mtu wa namna gani.
Kwamba ni Yule aliyeokoka na analiishi neno la Mungu.

TWENDE SASA KATIKA SOMO LETU

2PETRO 1:3-4
Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe.

Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa.

*******************

Uweza wa Mungu na Uungu  umetupatia sisi wateule kila kitu kitakachotusaidia kuwa wazima na watakatifu ndani yetu.
Uungu na uweza wa Mungu unatupa sisi uzima kwakuwa sisi wateule tunae mwombezi kwa Baba ambae ni Yesu Kristo mwenye haki.
Yeye alikuja ili tuwe na uzima tena tuwe nao tele.
Sasa uzima unatoweka kwetu kwaajili ya dhambi na ile dhambi ikishatakasika kwetu kwa damu yake basi uzima hurejea tena pamoja na utakatifu.

Uweza wake na Uungu wake ndivyo vilivyoweza kufanya namna ya yeye mwenyewe kuziacha mbingu na kuja duniani kutuokoa ili tuwe watakatifu.

Na kwa huo uzima na utakatifu akatukirimia ahadi kubwa mno na za thamani ili kwa hizo ahadi sasa tupate kuwa washirika wa tabia ya Uungu wake.
BWANA YESU ASIFIWE SANA.

Kwa ahadi zilizopo katika neno la Mungu sisi tunapata kuwa washirika wa ule Uungu na uweza wake.

Kuwa mshirika wa kitu ni kwamba mnakuwa kitu kimoja katika utendaji wa mambo yote hususani ni biashara au jambo lolote mnaloshirikiana kulifanya.
Sasa sisi tunakuwa washirika wa Uungu wake kwa kutamka vitu vikawa kama tunavyotamka.

TABIA YA UUNGU.

Tabia ya Uungu ni ile hali ya Mungu kufanya mambo bila mipaka na kwa wakati wowote bila kuzuiliwa na hali yoyote.
Sasa Mungu anasema sisi tunakuwa washirika wa tabia hiyo.
Na hiyo tabia ya Uungu inatusaidia sisi kuokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa.
Hiyo ni tabia ya Uungu na tukishakuwa nayo tutaishinda dunia maana Mungu hatendi dhambi wala hana tamaa ya kumuingiza katika dhambi.
BWANA YESU ASIFIWE

ISAYA 55:11
ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.

********************

Hii ni tabia ya Uungu ambayo hata sisi ni washirika wa hiyo ya kwamba akitamka neno lake ni lazima lifanye kama alivyosema na halimrudii bure.
Hii tabia imo ndani yetu pia.
BWANA YESU ASIFIWE SANA

YEREMIA 32:27
Tazama, mimi ni BWANA, Mungu wa wote wenye mwili; je! Kuna neno gumu lo lote nisiloliweza?

******************

Hakuna neno Mungu asiloliweza na huo uweza wake wa kutokushindwa jambo lolote ameuweka ndani yetu na sisi ni washirika wa huo.
NAMPENDA SANA YESU

MWANZO 1:26
Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.

********************

Ili kuthibitisha kwamba tu washirika wa tabia yake na uweza wake aliamua kutuumba kwa sura na mfano wake.
Akasema tutawale vyote.

Utisho wowote uliopo au unaotokea hapa duniani sisi tuna nguvu za kuufadhaisha.
Na wakati tunapotaka kuufadhaisha na kuunyong'onyeza huwa tunautiisha kwa jina la Yesu.
Sasa lile jina la Yesu (Mungu) ni vitu ambavyo vipo ndani yetu.
Unapomkemea pepo kwa jina la Yesu katika ulimwengu wa Roho huyo pepo huwa hakuoni wewe bali anaona sura ya Yesu ndiyo maana Hana namna yoyote ya kusimama na kujitunisha.
Sisi tunasimama kama Mungu hapa duniani kwa kuwa washirika wa ile tabia yake.
BWANA YESU ASIFIWE.

UWEZA WAKE

LUKA 10:19
Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.

********************

Ule uweza wake sasa na nguvu na mamlaka akaviweka kwetu ili tupate kuwa na tabia yake kabisa.
Anasema hakuna asiloliweza na wote tuliomwamini hatuna mashaka na uweza wake.
Kama yeye anavyoweza yote na sisi akatupatia uweza wa kuharibu nguvu zote za yule adui.
Tunakuwa washirika kamini.
BWANA YESU ASIFIWE

THAMANI YA MTEULE

WAEBRANIA 1:13-14
Je! Yuko malaika aliyemwambia wakati wo wote,Uketi mkono wangu wa kuumeHata nitakapoweka adui zako chini ya nyayo zako?

Je! Hao wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu?

******************

Yesu ni bora kuliko Malaika na biblia inatuambia kwamba yeye amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao.

Jina alilorithi ni jina YESU
halafu alilirithi kutoka kwa Baba.
Inamaana kumbe hilo jina siyo lake kwamaana huwezi ukarithi chakwako bali unarithi kilicho cha mwingine ili kiwe chako.
Jina ni la Baba kwa hiyo Mungu Baba ni Yesu.

Kama yeye ni bora kuliko malaika kwaajili ya hilo jina halafu hilo jina akatupa sisi inamaana sisi ni bora kuliko malaika.
malaika wapo na ni roho watumikao kutuhudumia sisi.
Yule aliyemwambia wewe ni mwanangu nimekuzaa ndiye bora kuliko malaika.
Na sisi tuliookoka WATEULE ni watoto wake.
Hivyo sisi ni bora kuliko Malaika.
BWANA YESU ASIFIWE SANA.

YOHANA 14:16-18
Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele;

Ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.

Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu.

***************
Akishamwachilia huyo Roho atatufundisha kulishika na kuliishi neno lake.
Halafu angalia kinachofuata sasa tukishaliishi neno.

YOHANA 14:23
Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake.

******************

Wote wakishafanya makao kwetu basi ule Uungu kamili (NAFSI ZOTE TATU) zinakuwa kwetu na kuwa washirika kamili kwa huo.

Ule uweza wa Mungu umewekwa ndani yetu automatically na una tenda kazi.

******************
YOHANA 15:7
Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa.

****************

Sisi tukishakaa ndani yake Yesu na kulishika neno lake tutaomba chochote naye atakitenda.
Huo uwezo wa kutamka mambo yakawa unakuwa ndani yetu.

Kwa maana nyingine ya ufafanuzi zaidi anamaanisha hivi
"NINYI MKISHAKUWA WAKAMILIFU NA KUISHI MAISHA MATAKATIFU MTAKUWA KAMA MIMI HIVYO MTAKUWA WASHIRIKA WA NGUVU ZANGU NA MTAKACHO TAKA KITAKUWA. "

Yani huo mfumo wa kwamba ukiwa mtakatifu uwe na mamlaka ya kutiisha kila kitu kwa jina la Yesu umetengenezwa ndani yetu na kwakuwa tunakuwa na chapa ya hilo jina basi vitu vyote vyenye majina ya kila namna vinajikuta havina nguvu ya kuhimili kwa kuwa hili jina Yesu linapita majina yote.

Kwanini haviwezi kuhimili??

YOHANA 17:22
Nami utukufu ule ulionipa nimewapa; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja.

****************

Haviwezi kuhimili nguvu za Mungu na utukufu wake maana vyote ameviweka kwetu.

Huwezi ukasimama na kusema kwamba wewe ni Mungu.
Lakini vyote vilivyo vya Mungu aliviweka ndani yetu.
Sisi ni copy yake kamili.

Jiulize ni kwanini unaweza ukamtamkia mtu maneno na yakampata?

METHALI 18:21
Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi;Na wao waupendao watakula matunda yake.

*****************
Kwa jinsi ulivyo mtakatifu ndivyo utatamka kwa kukataa uharibifu na kutamka mema na yakawa hivyo hivyo.
Lakini kwa jinsi unavyokuwa na uovu ndivyo ukitamka uharibifu na laana vitatokea kwasababu umemtii baba wa hivyo kwa viwango vinavyostahili.

YOSHUA 6:27-26
Naye Yoshua akawaapisha kiapo wakati ule, akasema, Na alaaniwe mbele za BWANA mtu yule atakayeinuka na kuujenga tena mji huu wa Yeriko; ataweka msingi wake kwa kufiliwa na mzaliwa wa kwanza wake, tena atayasimamisha malango yake kwa kufiliwa na mtoto wake mwanamume aliye mdogo.

Basi BWANA alikuwa pamoja na Yoshua; sifa zake zikaenea katika nchi ile yote.

******************

Mtumishi wa Mungu Yoshua alitamka kwa kinywa chake na kulaani yeyote atakayejaribu kuijenga Yeriko.
Yoshua alisimama akatamka na kwakuwa Mungu alikuwa ndani yake basi yale maneno ya laana yakathibitika.

1WAFALME 16:34
Katika siku zake, Hieli Mbetheli akajenga Yeriko; akatia misingi yake kwa kufiwa na Abiramu mzaliwa wake wa kwanza, na kuyaweka malango yake kwa kufiwa na mwana wake mdogo Segubu; sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa Yoshua mwana wa Nuni.

****************

Kule mwanzoni Yoshua alitamka mwenyewe na kinywa chake.
Lakini huku mwishoni biblia inatuambia
""Sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa Yoshua mwana wa Nuni"

Kumbe aliyesema siku ile na kulaani alikuwa ni Mungu siyo Yoshua.

Wakati wa Agano la kale Mungu alikuwa anamteuwa mtumishi wake wa kuwa mshirika wa Uungu wake lakini kwa sasa kila anayekuwa ameokoka (MTEULE) anaweza kuwa mshirika wa tabia yake ya Uungu.
BWANA YESU ASIFIWE SANA

NGUVU ZETU ZIKO WAPI SASA?

Tumeona namna ambavyo sisi tulivyo bora kuliko malaika,
Lakini sasa utashangaa malaika wanaweza kufanya mambo makubwa zaidi yetu tena ya kustaajabisha.
Malaika anaweza kuja akasimama kama Mungu kabisa na nguvu zote za Mungu akafanya alichoagizwa halafu akaondoka.

WARUMI 3:23-24
kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;

wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu;

****************

Dhambi ndiyo iliyotuondolea ule utukufu wa Mungu na uwezo wa kufanya mambo ya Kiungu ili tuwe washirika halisi wa ule Uungu wake.

Utukufu na uweza ambao Yesu alipewa na Baba na ukamwezesha kufanya mambo makubwa ya kuishangaza dunia, anasema ametupatia sisi lakini ukapungua kwetu kwaajili ya dhambi.

Malaika wanatuzidi sisi kwasababu wao hawatendi dhambi.
Ule utaratibu wa Mungu kumtembelea Adamu bustanini kila siku na kuongea naye uliishia pale Adamu alipotenda dhambi.

Lakini kwa sasa tunahesabiwa haki bure kwa njia iliyo katika ukombozi wa Kristo Yesu lakini bado hatuwezi kuishi na ile haki.
Tunakuwa watu wa dhambi kila wakati na utukufu wake kwetu unazidi kupungua na tunashindwa kuwa washirika wa ule Uungu kwaajili ya dhambi na kushindwa kuishi maisha matakatifu.

BWANA YESU AKUBARIKI SANA

#Powered_By_Holly_Spirit

1 comment: