Wednesday, 13 June 2018

YOTE YALIKWISHA KWA KAZI YA MSALABA.

BWANA YESU ASIFIWE NA KUPEWA UTUKUFU WOTE.

Leo Roho Mtakatifu amekusudia kabisa kutufundisha namna ambavyo mtu unaweza ukawa huru ndani ya Kristo.

Somo letu lina kichwa kinachosema,

YOTE YALIKWISHA KWA KAZI YA MSALABA.

Neno letu la msingi katika mafundisho yetu ni

YOHANA 8:36
Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.

*****************
Haya maneno aliyaongea Bwana wa mabwana Yesu Kristo wakati akiwaambia wale Wayahudi kwamba wamekuwa watumwa wa dhambi hivyo yeye akiwa ni mwana wa Mungu anao uwezo wa kuwaweka huru tena huru kwelikweli.

Anasisitiza kwamba anakuweka huru kwelikweli ili ukishaingia ndani yake na pia yeye akishaingia ndani yako usije ukahisi kwamba kuna namna hauko huru kwa kufungwa kwa namna yoyote.

2WAKORINTHO 5:17
Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.

*****************

Unapokuwa ndani ya Kristo yaani unapo okoka na kumpokea katika maisha yako huwa unafanyika kiumbe kipya kabisa.
Mambo yote ya kale yanakwisha na kuwa mapya kabisa.
Usije ukawa na wasiwasi wa kuwaza tena kwamba bado unasumbuliwa na mambo ya nyuma.
Unakuwa kama Adamu pale Edeni kabla hajala lile tunda.
Sijui kama unaelewa maana ya kitu kuwa kipya!
Unakuwa mpya bila mambo ya kurithi ndani yako, laana za mabibi na mababu, dhambi ya asili, na kila namna iliyo kinyume na mpango wa Mungu katika maisha yako.

ISAYA 61:1
Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu BWANA amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao.

****************

Zile habari zote ulizokuwa unazisikia zikiongea ndani yako za kukukatisha tamaa zinakwisha, sauti nyingi zilizokuwa zinasema ndani yako ya kwamba wewe ni tasa, wewe ni masikini, wewe hutaolewa au kuoa, wewe hutafanikiwa, au huna tumaini zote zinakuwa zimekwisha kabisa na zinabaki sauti za ushindi tu ndani yako ambazo ndizo habari njema anazozihubiri Yesu Kristo ndani yako.

Ile hali ya kuvunjika moyo ndani yako ya kutokuona kama una tumaini lolote la yale unayopitia yeye alikuja kuyaganga na kuwa tumaini lisilo na mipaka ndani yako.

Ulikuwa umetekwa na nguvu za giza, nafsi yako haikuwa huru, haukuwa na amani moyoni mwako na nafsi kuhangaika kwa kutokujuwa ni wapi utapitia lakini yeye alikuja na uwezo mkubwa wa kukuweka huru kweli kweli.

Ulikuwa umefungwa na wachawi, umefunikwa kwenye chupa, ufahamu wako umefungwa, huna maarifa yoyote ya kujikwamua katika huo umbumbumbu,
Sasa kitendo cha kumpokea Yesu tu unafunguliwa.

MATHAYO 27:26
Ndipo akawafungulia Baraba; na baada ya kumpiga Yesu mijeledi, akamtoa ili asulibiwe.

****************

Unapompokea tu Yesu unakuwa umefunguliwa kwasababu yeye alipigwa mijeledi ili wewe ufunguliwe.
Ukishakuwa ndani yake unafunguliwa na unakuwa huru kweli kweli,
Baraba alipofunguliwa hakufungwa tena hivyo usije ukaokoka halafu bado katika fikra zako ukawaza kwamba umefungwa tena.
Vile vifungo vyote vinakuwa vimeondoka ndani yako na unakuwa huru kabisa.

1PETRO 2:24
Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa.

**************

Kupigwa kwa Yesu tu sisi tulipona pale pale na magonjwa yalikimbia,

LAKINI UNAWEZA UKAJIULIZA JE, KAMA NI HIVYO NI KWANINI NIMEOKOKA LAKINI BADO MAGONJWA YAPO?

YOHANA 8:32
tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.

**************

Nimekufahamisha vizuri sana namna ambavyo ukiokoka unakuwa huru na vifungo vya namna zote katika maisha yako.

Sasa ili uwe huru ni mpaka uifahamu hiyo kweli ya Mungu ili ikuweke huru.
Je, kweli ya Mungu ni ipi?

YOHANA 17:17
Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.

****************

Ili utakasike sasa na kuwa kiumbe kipya kabisa ni lazima ulielewe neno la Mungu kwa viwango vikubwa.

Unavyozidi kuielewa Kazi ya msalaba na kusudi la Bwana Yesu kufia msalabani pamoja na thamani ya mauti yake bila kuwa na Shaka moyoni mwako ndivyo unavyoelekea kuwa huru kabisa katika maisha yako.

Ndiyo maana unakuta mtu mwingine alikuwa na magonjwa sugu na ya kurithi lakini hayakupona siku alipo okoka ila kadri anavyozidi kusoma neno na kulikiri moyoni mwake kwa imani anajikuta amepona hata ukimuliza alipona lini anakuwa hajui bali alikuja kushangaa tu haumwi tena.

Nilisikiliza ushuhuda wa dada mmoja alizaliwa akiwa na ugonjwa ulioshindikana hospitali zote na yeye alikuwa muislamu.
Ule ugonjwa ulikuwa tishio hata kwa familia yake nzima na ulipelekea wakaokoka wote.
Japo waliokoka lakini hakupona pia.
Lakini Yule dada alikuwa anahudhuria kila mkutano wa injili uliokuwa ndani ya uwezo wake kuhudhuria.
Anasema siku moja alisafiri kutoka Arusha kuelekea Moshi kwenye semina ya neno la Mungu.
Lakini alikosa usafiri.
Aliazimia moyoni mwake kutokuukosa akaamua kusafiri hata usiku ili kesho yake aamkie kwenye semina.
Alifanikiwa kufika usiku ule akakesha kwenye kamati ya maombi ili kesho yake akaombewe na mchungaji lakini alipoamka asubuhi alijikuta siyo mgonjwa tena alishapona kabisa.

Ni ugonjwa aliozaliwa nao na hakuwahi kumaliza siku nzima bila kuugua nusu ya kufa kwa kipindi chote alivyoishi mpaka kufikia umri wa miaka 15 ndipo akapokea uponyaji.

Unapookoka tu huwa unapona na ya kale yanakwisha unakuwa mpya kabisa.
Ile kweli ambayo ni neno la Mungu ndani yako ndivyo vinakufanya uamini uponyaji.
Hata kama unajiona bado ni mgonjwa ujue huo ni uongo wa shetani tu ili usiamini hiyo kweli ambayo ni NENO (Yesu) ndipo uwe huru.

1PETRO 1:18-19
Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu;

bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo.

*********************

Huwezi ukaokoka halafu ukatafuta tena ibada za ukombozi eti ukakombolewe.
Hapo unamaanisha ukombozi aliokukomboa Yesu akasema umekuwa kiumbe kipya na ya kale yote yamepita kwamba umeharibika.
Hutakuwa huru maana hujaitambua Kazi ya msalaba.
Ule ukombozi hauharibiki.
Ametaja dhahabu isiyoharibika kwa namna ya kibinadamu lakini akaifananisha na thamani ya ukombozi aliyokukomboa nayo kwamba ukivilinganisha bado hiyo dhahabu inaonekana inaharibika.

Ulipompokea tu ulikombolewa wala usije ukamaliza miaka kadhaa halafu ukadhani ule ukombozi umeharibika ukataka kutafuta tena namna ya kujikomboa.
Hapo utakuwa umeidharau Kazi yake ya ukombozi na hujaifaimu ile (KWELI, NENO, YESU) ili likuweke huru.

ANAYESTAHILI KUTAFUTA NAMNA YA KUFUNGULIWA, KUWEKWA HURU AU KUKOMBOLEWA NI AMBAYE HAJAOKOKA, NA ANAPO OKOKA TU ANAWEKWA HURU, ANAFUNGULIWA NA KUKOMBOLEWA NA ANAKUWA KIUMBE KIPYA.

WARUMI 3:25
ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa;

****************

Baada ya mwanadamu kufarakana na Mungu pale Edeni Yesu alikuja kutupatanisha nae tena kwa njia ya wokovu.
Dhambi zote ulizozifanya huko nyuma, laana za mababu na mabibi zinakwisha zote unapompokea Yesu kwa njia ya kuokoka.

WAGALATIA 3:13
Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti;

******************

Kitendo cha yeye kutundikwa tu pale msalabani laana zote zilikwisha maana yeye alifanyika laana akalaaniwa yeye ili sisi tuondokane na laana.
BWANA YESU ASIFIWE SANA.

1WAKORINTHO 1:18
Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.

*****************

Unapotafuta namna nyingine ya kujiondolea laana baada ya kuokoka unakuwa unapuuza Kazi ya msalaba ambayo ni nguvu ya Mungu.
Huwezi ukaanza tena kuvunja laana za kale na wakati neno linasema ya kale yamepita tazama sasa yamekuwa mapya mtu anapokuwa ndani ya Kristo.
Unapo okoka yote huwa mapya.

Ni jambo la kushangaza sana mtu uliyeokoka unafanya maombi ya kuvunja laana na wakati kitendo cha wewe kuwa katika Kristo ulipokiri ulifanyika mpya kabisa na ya kale yalikwisha.

WAKOLOSAI 1:13
Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake;

***************

Alikutoa katika nguvu za giza.
Na baada ya kukutoa hakukuacha njiani bali alikuhamisha na kukuingiza katika ufalme wake.
Kuna falme mbili katika ulimwengu wa roho.
Upo ufalme wa shetani (ufalme wa giza)
Na pia upo ufalme wa Mungu (Ufalme wa nuru)

Katika ngome yoyote ya ufalme kunakuwa na ulinzi imara sana.
Tuchukulie mfano tu kama ikulu ya Raisi ambaye ni mwanadamu huwa mtu hawezi kuingia.
Sasa ufalme wa Mungu mwenye nguvu itakuwaje?
Sasa unapo okoka Yesu anakupeleka kwenye ufalme wake ukiwa mpya kabisa, magonjwa,kufadhaika,kukata tamaa, laana za mabibi na mababu na kila aina ya uharibifu huwa unaviacha huko kwa shetani.
Anakuingiza kwenye ufalme wake ukiwa kiumbe kipya kabisa.
Unavyotafuta tena kukombolewa unamaanisha kwamba katika ufalme wake hakuna ulinzi hivyo shetani aliwazidi nguvu wale walinzi akakuteka tena akakurudisha kwenye ufalme wake.
Umemdharau Yesu na ufalme wake.
Anasema akikuweka huru utakuwa huru kwelikweli ndani ya ufalme wake lakini wewe unabisha kwamba hakuweza kukuweka huru hivyo unatafuta tena kufunguliwa.

YOHANA 19:28
Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, Naona kiu.

******************

Yote yalikwisha kwa kazi ya msalaba,
Kwa kukiri tu na kuamini moyoni mwako kwamba alikufa kwa ajili yako na kufufuka huwa yote yanakwisha.

WAEBRANIA 10:9-10
ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili.

Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.

******************
Aliondoa lile agano la mashaka,agano aliloliweka la pili ni la kukutakasa kabisa na lilifanyika mara moja tu.
Hivyo unapo okoka mara moja tu unaliishi na kuendelea kuwa na uhalali wa kuitumia damu ya Yesu kujitakasa.

WARUMI 5:1
Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo,

*******************

Ili uamini kwamba umehasabiwa haki ni lazima uwe na imani na ile damu ya Yesu.
Unapotubu kwa kumaanisha utahesabika mwenye haki mbele za Mungu utakapokuwa na imani na ile damu kwamba imekutakasa na kuwa mtakatifu.
Usipoamini na kuwa na imani kwamba umesamehewa ujue bado utakuwa na dhambi kwa kuwa na mashaka na uwezo wa damu ya Yesu kukutakasa.

Endelea kukiri kupona na kumfahamu Yesu zaidi kwamba anasema nini juu ya hilo unalopitia nawe utakuwa huru.
Kuwa na imani na neno lake.
Yeye si mwanadamu hata aseme uongo.
Neno lake ni kweli.
Acha kusikiliza sauti za adui ndani yako zinazokuambia kwamba hujapona,kwamba wewe ni dhaifu au muda wote unaomba mbona hujafanikiwa.
Mjibu kwa neno, hizo sauti zijibu kwa neno.
Mwambie Mungu hachelewe wala hawahi, mwambie nimewekwa huru kweli kweli.
Zile sauti ndizo zinazokufanya usiiamini ile kweli ili ikuweke huru.

BWANA AKUBARIKI KWA JINA LA YESU KRISTO.

#Powered_By_Holly_Spirit

1 comment:

  1. Asante kwa Neno. Yesu alimaliza Kazi pale msalabani. Hakuna ukombozi mwingine tena.

    ReplyDelete